NDAIRAGIJE AJIAMINI KABLA YA YANGA, POINTI 42 ZINATUTOSHA…….
KOCHA Mkuu wa TRA United, Etienne Ndairagije, amesema timu yake itaingia uwanjani ikiwa na lengo la kuendelea kuonyesha ubora wake na kuitambulisha klabu hiyo, badala ya kufikiria nafasi za juu ambazo zimekuwa zikizungumzwa na wadau kuelekea mwisho wa msimu.
Akizungumza kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Yanga, Ndairagije amesema tangu mwanzo wa msimu hawakuwa na malengo ya kumaliza katika nafasi ya nne au kufuzu michuano ya kimataifa, bali walijipanga kuhakikisha TRA United inajijengea heshima baada ya kupanda Ligi Kuu msimu huu.
Kocha huyo ameeleza kuwa pointi 42 walizokusanya hadi sasa ni ushahidi kuwa timu yake imekuwa ikifanya vizuri, jambo linaloonyesha kuwa imefanikiwa kufikia malengo yake ya msingi.
“Sisi hatukuwa na malengo ya kimataifa wala kumaliza nafasi ya nne kama watu wanavyozungumzia. Lengo letu la kwanza lilikuwa ni kuitambulisha TRA United baada ya kupanda daraja msimu huu. Hata mechi ya leo tunaendelea na lengo hilo kwa kuonyesha ubora wa timu yetu,” alisema Ndairagije.
Alipinga vikali mtazamo kwamba TRA United imekuwa ikipata ugumu inapocheza mechi za ugenini, akisisitiza kuwa rekodi yao ya msimu inaonyesha timu imekuwa na ushindani bila kujali inapocheza.
TRA United leo itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, huku ikisaka kuendelea kuonyesha kiwango chake dhidi ya mabingwa hao.