Jesus Moloko Kuibukia Angola
ALIYEKUWA winga wa Mbeya Kwanza iliyoshiriki Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026, Mkongomani Jesus Ducapel Moloko, yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na Klabu ya Primeiro de Maio inayoshiriki Ligi Kuu ya Angola maarufu Girabola.
Nyota huyo aliyejiunga na Mbeya Kwanza katika dirisha dogo la Januari 2026, hivi karibuni aliondoka kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo mjini Tabora ikijiandaa na mechi ya Play-Off, kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Moloko amesema aliondoka katika kambi hiyo kwa ajili ya kushughulikia changamoto mbalimbali alizokuwa nazo, japo suala la kujiunga na timu nyingine akisema kwa sasa bado, licha ya kukiri mkataba wake tayari umemalizika..
“Nilisaini mkataba wa miezi sita na Mbeya Kwanza na nipo huru kujiunga na timu nyingine msimu ujao, nashukuru kwa sapoti kubwa niliyoipata toka mwanzo, japo hatujaweza kufikia malengo ya kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja,” amesema Moloko.
Nyota huyo aliyewahi kuitumikia Yanga kuanzia Agosti 13, 2021 hadi Januari 28, 2024, wakati alipojiunga na kikosi hicho akitokea AS Vita ya kwao DR Congo, alijiunga na Mbeya Kwanza Januari 2026, baada ya kuachana na AS Kigali kutoka Rwanda.
Moloko alijiunga na AS Kigali Agosti 28, 2025, baada ya kuachana na ES Mostaganem ya Algeria, ingawa hakudumu nayo baada ya kuondoka Januari 2026, huku akichezea timu mbalimbali zikiwemo za Diyala SC ya Iraq na Al Sadaqa Shahat SC ya Libya.