Habari za michezo

Rashford Uso Kwa Uso Na Rafiki Yake Wa Utotoni

Vardo June 30, 2026 5:58 pm

ATLANTA, MAREKANI: MARAFIKI wa tangu utotoni, Marcus Rashford na Axel Tuanzebe wanatarajiwa kukutana katika mechi ya Kombe la Dunia itakayozikutanisha England na DR Congo katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia, mechi ambayo itachezwa leo, saa 1:00 usiku.

Wawili hao waliwahi kuwa marafiki wa karibu tangu utotoni, baada ya kusoma pamoja katika Shule ya Aston on Mersey School huko Greater Manchester, England.

Baadaye wote walipitia akademi ya Manchester United na hata kucheza pamoja katika kikosi cha wakubwa wakiwa vijana. Hata hivyo, Tuanzebe baadaye alibadili uamuzi wake wa kimataifa na kuamua kuiwakilisha DR Congo baada ya kukosa nafasi ya kudumu katika kikosi cha England.

Rashford naye anaendelea kuwa miongoni mwa nyota muhimu wa England, na anatajwa huenda akaanza katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Thomas Tuchel, baada ya kuanza kwenye baadhi ya mechi kama mchezaji wa akiba katika hatua za makundi.

Wawili hao hawakuwa peke yao waliotoka katika shule hiyo kufanikiwa kuwa wanasoka wa kulipwa, kwani wengine ni Jimmy Dunne na Tosin Kehinde, ambao pia walicheza soka la kulipwa.

Dunne kwa sasa anaichezea Queens Park Rangers na pia amechezea timu ya taifa ya Ireland, huku Kehinde akicheza katika mataifa mbalimbali  Ulaya na kwa sasa akiichezea klabu ya Bandirmaspor ya Uturuki.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na hisia kali, kwani itaweka marafiki wa zamani katika nafasi tofauti za ushindani wa kimataifa, ambapo Rashford atakuwa akitafuta mabao kwa England na Tuanzebe akijaribu kuyazuia.
Nini Kinachifuata Usyk Kuachia Mikanda Mitatu Meridianbet Yaandika Hadithi Mpya Ya Matumaini Kwa Wasichana Katavi