Mo Dewji Atoa Neno Paredi La Ubingwa Simba
RAIS wa Heshima wa Simba na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, amesema mafanikio ya kutwaa Kombe la CRDB yanapaswa kuwa chachu ya kuipeleka timu hiyo kwenye mafanikio makubwa zaidi.
Bosi huyo ametoa kauli hiyo leo kwa njia ya simu wakati wa kilele cha paredi ya ubingwa kilichofanyika Coco Beach, Dar es Salaam, ambapo maelfu ya mashabiki wa Simba walikusanyika kusherehekea taji hilo.
Akizungumza na mashabiki, Mo ameanza kwa kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na wanachama kwa mchango wao uliowezesha Simba kumaliza msimu ikiwa na kombe.
“Nawapongeza sana mashabiki wa Simba, nawapongeza viongozi, nawapongeza wachezaji na kila Mwanasimba kwa mafanikio haya. Asanteni kwa kuendelea kuiunga mkono timu yetu,” amesema.
Mwekezaji huyo amesema, pamoja na kufurahia Kombe la CRDB, kiu yake kubwa sasa ni kuona Simba ikifanikiwa kutwaa taji la Afrika iwe Ligi ya Mabingwa au Kombe la Shirikisho Afrika.
Kauli hiyo imepokewa kwa shangwe na maelfu ya mashabiki waliokuwa Coco Beach huku wakipaza sauti za kuunga mkono azma hiyo.
Mo amehitimisha salamu zake kwa kuwaombea kila la heri Wanasimba, akisisitiza kuwa kwa umoja na mshikamano klabu hiyo inaweza kufikia malengo makubwa zaidi misimu ijayo.