Kapombe Aahidi Mataji Zaidi Msimu Ujao
NAHODHA wa Simba, Shomary Kapombe amewashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi leo Jumapili katika paredi ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, huku akisema sapoti hiyo ikiendelea, msimu ujao watafanya vizuri zaidi.
“Kwa niaba ya wachezaji, kwanza napenda kuwashukuru mashabiki na wanachama wote ambao mmejitokeza kwa wingi. Hatukutarajia kuona umati mkubwa kama huu. Asanteni sana kwa kutuunga mkono,” amesema Kapombe.
Nahodha huyo amesema paredi ya Simba imeweka rekodi kwa muda mrefu wa kusherehekea, akieleza kuwa msafara huo ulidumu kwa takribani saa 10.
“Paredi yetu imetumia saa 10 na bado watu wanaendelea kushangilia. Hii inaonyesha namna ambavyo mnaipenda Simba na mnavyothamini mafanikio ya timu yenu,” amesema.
“Msimu hatukuanza vizuri, lakini tumemaliza vizuri. Hilo limetokana na ushirikiano wa kila mmoja ndani na nje ya uwanja,” amesema.
Nahodha huyo amewaomba mashabiki kuendelea kuipa timu sapoti kama walivyoonyesha katika paredi hiyo, akisisitiza Simba ina malengo makubwa zaidi katika msimu ujao.
“Tunaomba jambo moja, kama mlivyokuwa nasi leo, msimu ujao muendelee kutusapoti kwa nguvu hizi hizi. Tukipata sapoti kama hii tunaamini tutafanya makubwa zaidi kuliko tuliyofanya msimu huu,” amesema mkongwe huyo ambaye yupo klabuni hapo tangu 2017.