Simba Yashinda Usajili, Mwalimu Abaki Kwa Mkopo Simba
UONGOZI wa Simba SC umefikia hatua muhimu katika mazungumzo yao na klabu ya Wydad AC pamoja na mshambuliaji wake, Selemani Mwalimu, kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo kuelekea msimu wa 2026/27, ambapo pande hizo zimekubaliana kwa kiasi kikubwa juu ya kuendelea kwake kubaki Msimbazi kwa mkopo.
Kwa mujibu wa taarifa za karibu na mazungumzo hayo, Mwalimu mwenyewe tayari ametoa ruhusa ya kusalia Simba, hatua ambayo imefungua mlango wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Simba na Wydad AC kuingia katika hatua za mwisho za kukamilisha dili hilo.
Inaelezwa kuwa sehemu kubwa ya makubaliano ya awali kati ya pande zote tatu imekwisha kufikiwa, na kilichosalia sasa ni mazungumzo ya mwisho kuhusu ada ya mkopo (loan fee) pamoja na baadhi ya masharti madogo madogo kabla ya dili hilo kutangazwa rasmi.
Chanzo cha karibu kimeeleza kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri bila mivutano mikubwa, hali inayoonesha nia ya pamoja ya kuhakikisha mchezaji huyo anaendelea kuitumikia Simba kwa msimu mwingine muhimu unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa.
Kwa upande wake, mtoa taarifa wa karibu na mchezaji huyo amesisitiza kuwa hakuna dalili za mabadiliko ya ghafla, akibainisha kuwa msingi wa makubaliano umeshajengwa na pande zote ziko kwenye njia sahihi ya kufanikisha dili hilo.
“Sehemu kubwa ya kila kitu imekamilika. Yamebaki mambo madogo ya klabu kwa klabu. Mchezaji mwenyewe ameshakubali kubaki,” kilieleza chanzo hicho.
Hatua hiyo imezidi kuongeza matumaini kwa mashabiki wa Simba, ambao sasa wanasubiri tamko rasmi la klabu kuthibitisha dili hilo, ambalo linaonekana kuwa limeiva na huenda likakamilika muda wowote kuanzia sasa.