Kisa Singida BS, Azam Yahaha Kwa Kitambala
AZAM inahaha kumrudisha kundini mshambuliaji wake, Jephte Kitambala ambaye amebakiza hatua chache kumalizana na Singida Black Stars iliyomchukua kwa jeuri ya fedha.
Kiwango alichoonyesha Kitambala kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba ndio kimebadilisha upepo huo, mabosi wa klabu hiyo wakiona Mkongomani huyo bado ana nafasi.
Ripoti ya kocha Florent Ibenge imeonyesha kumuhitaji zaidi Jean-Jacques Ngita kuendelea kubaki Azam, lakini matajiri wa klabu hiyo wanaona Kitambala ana kitu kikubwa akistahili kukitumikia kikosi hicho.
Wakati Azam wakibishana kwa hoja, Singida haikusubiri, ikashusha ofa kubwa kwa mshambuliaji huyo na uongozi wake ukakubali kila kitu na sasa dili lipo hatua za mwisho kumalizika.
“Tutamalizana na Singida kwani wametupa ofa nzuri, kuna uwezekano mkubwa sana Kitambala atakwenda huko, jambo zuri ni kwamba mkataba wake na Azam umemalizika, tunawashukuru,” alisema bosi anayemsimamia Kitambala.
“Azam tumeona wanabishana, viongozi wanamtaka Kitambala lakini shida inaonekana ipo kwa kocha (Ibenge) ameonyesha anataka kubaki na Ngita, sasa wanakuja viongozi wanasema tuache ofa ya Singida, hiyo itakuwa ngumu.”
Msimu uliomalizika, Kitambala amefanikiwa kufunga mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara, akiwa na asisti moja, ni mchezaji wa tatu kwa ufungaji ndani ya Azam nyuma ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyemaliza na mabao 15 na Iddi Seleman ‘Nado’ mwenye mabao nane.