Yanga SC

Yao Aweka Masharti Kabla Ya Kuamua Hatma Yake

Vardo July 8, 2026 2:06 pm

BEKI wa kimataifa wa Yanga, Yao Kouassi, huenda akawa mmoja wa wachezaji watakaotikisa dirisha hili la usajili baada ya kumalizika kwa mkataba wake na mabingwa hao wa Tanzania, huku hatma yake ikiwa bado haijajulikana.

Taarifa zinaeleza kuwa hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita, Yanga ilikuwa bado haijaanza mazungumzo rasmi ya kuongeza mkataba wa beki huyo, hali iliyozipa nafasi klabu nyingine kuanza kuonyesha nia ya kumsajili.

Inaelezwa kuwa tayari Yao amepokea ofa nono kutoka klabu moja ya nchini Misri, ambayo ipo tayari kumsajili kwa masharti mazuri kuelekea msimu ujao.

Hata hivyo, beki huyo ameomba kupewa muda zaidi na klabu hiyo ya Misri, akitaka kwanza kusubiri kuona kama Yanga itawasilisha ofa ya kumbakisha kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu mustakabali wake.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na mchezaji huyo, Yao bado anaipa kipaumbele Yanga kutokana na uhusiano mzuri alioujenga ndani ya klabu hiyo pamoja na mafanikio aliyoyapata tangu alipowasili Jangwani.

Aidha, imeelezwa kuwa nyota huyo ana mapenzi makubwa na Tanzania kutokana na mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa mashabiki na mazingira aliyokutana nayo tangu alipojiunga na Yanga.

Kwa sasa, kila kitu kinasubiri uamuzi wa Yanga. endapo mabingwa hao watamwekea mezani ofa itakayomridhisha, Yao anaweza kuendelea kubaki Jangwani. Lakini ikiwa hilo halitatokea, beki huyo yupo tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka nchini Misri.

Tumia Bet Builder Upate Odds Kubwa na Meridianbet Leo