Samatta Aaga Taifa Stars, AFCON 2027 Atabaki Jukwaani
KABLA ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda, nahodha wa muda mrefu wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa, hivyo hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachowakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo ya kihistoria.
Samatta anahitimisha safari ya takribani miaka 15 akiwa na Taifa Stars, kipindi kilichojaa mafanikio, changamoto na kumbukumbu nyingi zilizoandika historia ya soka la Tanzania.
Katika kipindi hicho, amekuwa mmoja wa wachezaji waliobeba taswira ya timu ya taifa ndani na nje ya uwanja, huku akivaa beji ya unahodha kwa takribani miaka 10.
Katika taarifa yake ya kustaafu, mshambuliaji huyo amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akieleza kuwa anajivunia kupata nafasi ya kulitumikia taifa lake kwa kipindi chote alichokuwa sehemu ya Taifa Stars.
Samatta amesema miongoni mwa mafanikio anayoyathamini zaidi ni kuiongoza Tanzania kufuzu fainali za AFCON mara tatu, pamoja na kushuhudia timu ikiandika historia ya kutinga hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza.
“Ninaamini huu ni wakati wa vizazi vipya kupewa nafasi ya kutufikisha kwenye hatua za juu zaidi,” amesema Samatta, akisisitiza kuwa anaondoka akiwa na imani kubwa kwa wachezaji wanaokuja kuendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Ameitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mchango wao katika maendeleo ya soka nchini na juhudi za kuijenga Taifa Stars kuwa timu yenye ushindani zaidi.
Kustaafu kwa Samatta kunahitimisha enzi ya mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa katika historia ya Taifa Stars. Ingawa hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshiriki AFCON 2027, urithi wake utaendelea kukumbukwa huku jukumu la kuendeleza mafanikio hayo likikabidhiwa kizazi kipya cha wachezaji.