KVZ Yajinoa Kagame Cup 2026
MABIGWA wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu wa 2025-2026, KVZ, imeanza mazoezi rasmi ya kujinoa kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup 2026).
Akitoa taarifa rasmi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Abduljalil Mohamed Salum, amesema baada ya kusherekea ubingwa, sasa timu imerudi kambini.
“Baada ya mapumziko mafupi tuliyoyapata ya kumaliza Ligi Kuu Zanzibar timu imeanza mazoezi na tunajiandaa kutangaza usajili mpya uliofanywa na timu,” amesema
Jalil amesema, timu hiyo imefanya usajili kwa kutoa wachezaji kila klabu kubwa kwani wanahitaji kuiwakilisha Zanzibar kimataifa kwa uzuri na sio vibaya.
Amesema, wanaamini kwamba wachezaji hao wataisaidia timu kufanya vizuri hivyo mashabiki waendelee kuiunga mkono KVZ.
Alieleza, kuwa mashine hizo zitaanza kazi katika michuano ya Kagame Cup na mashindano ya klabu bingwa barani Afrika.
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limethibitisha jumla ya timu 11 kufikia sasa zitachuana kuwania taji hilo ikiwemo Simba, APR FC na Rayon Sport zote za Rwanda, Vipers SC (Uganda), Al Hilal SC na El Merriekh SC (Sudan), Gor Mahia (Kenya), Mogadishu City (Somalia), Jamus SC (Sudan Kusini), FC Garde Républicaine (Djibouti) na KVZ FC (Zanzibar).