Singinda Black Stars Yafanya Usafi, Aucho Yamkuta
UONGOZI wa Singida Black Stars unaendelea na mipango ya kukifanyia maboresho makubwa kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa mashindano, huku baadhi ya wachezaji wakitajwa kuwa kwenye mpango wa kuachana na klabu hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa viongozi wamefikia uamuzi wa kufanya mabadiliko katika kikosi kwa kuwaachia baadhi ya nyota waliokuwa sehemu ya timu hiyo msimu uliopita, ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya watakaoongeza ushindani.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuondoka ni kiungo wa kimataifa wa Uganda, Khalid Aucho, ambaye mkataba wake na Singida Black Stars unadaiwa kufikia tamati.
Mbali na Aucho, taarifa hizo zinaeleza kuwa klabu hiyo inapanga pia kuachana na Morice Chukwu, Horso Mwaku pamoja na Idriss Diomande, katika hatua ya kukisuka upya kikosi kwa ajili ya msimu ujao.
Inadaiwa maboresho hayo yanalenga kujenga timu yenye ushindani zaidi kwa kuongeza wachezaji wapya watakaokidhi mahitaji ya benchi la ufundi na kusaidia kufikia malengo ya klabu hiyo.
Hata hivyo, hadi sasa uongozi wa Singida Black Stars haujatangaza rasmi kuhusu hatma ya wachezaji hao, huku mashabiki wakisubiri kuona hatua zitakazochukuliwa na klabu hiyo katika kipindi hiki cha usajili.