Simba, Yanga Wapewe Tahadhari! Azam Yatenga Bilioni 8
KATIKA kuhakikisha wanaingia kwa nguvu msimu wa 2026/27, uongozi wa Azam FC umetenga bajeti ya takribani Sh bilioni 8 kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya watakaokiimarisha kikosi hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa Azam FC imeweka mkakati maalumu wa kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake kwa lengo la kuongeza ushindani katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine msimu ujao.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari, uongozi wa klabu hiyo unapanga kuachana na baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao hawapo tena kwenye mipango ya benchi la ufundi, hatua itakayotoa nafasi kwa nyota wapya kujiunga na kikosi hicho.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa usajili huo utalenga kuziba mapungufu katika maeneo mbalimbali ya kikosi, huku lengo likiwa ni kujenga timu imara yenye uwezo wa kushindana kwa kiwango cha juu ndani na nje ya nchi.
“Azam FC imejipanga kufanya usajili wa kiwango cha juu ili kuimarisha maeneo yenye mapungufu.
Lengo kuu ni kushindana bega kwa bega na Simba SC na Yanga SC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine,” alisema mtoa taarifa huyo.
Imeelezwa kuwa dirisha hili la usajili linatarajiwa kuwa miongoni mwa makubwa zaidi katika historia ya Azam FC, kutokana na uwekezaji mkubwa uliopangwa kufanywa na uongozi wa klabu hiyo.
Iwapo mipango hiyo itatekelezwa kama ilivyopangwa, Azam FC itakuwa na kikosi kipya chenye ushindani mkubwa, huku matarajio yakiwa ni kurejesha makali yake na kutoa upinzani mkali kwa Simba SC na Yanga SC katika harakati za kutwaa mataji msimu wa 2026/27.