Fadlu Aikataa Yanga, Maongezi Yagonga Mwamba
ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba SC, Davis Fadlu, ameshindwa kujiunga na Yanga SC baada ya mazungumzo baina ya pande hizo mbili kuvunjika bila kufikia makubaliano ya mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Afrika Kusini, tofauti katika baadhi ya vipengele vya mkataba, hususan suala la bonasi zinazohusiana na mafanikio ya timu, zimeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zilizofanya mazungumzo hayo kushindikana.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa licha ya pande hizo kuonyesha nia ya kufanya kazi pamoja, kushindwa kufikia muafaka kwenye masharti muhimu kumeifanya Yanga kuachana na mpango wa kumsajili kocha huyo.
“Kutokana na hali hiyo, dili la kumpeleka Fadlu Yanga limefutika rasmi. Kocha huyo hatakuwa sehemu ya mipango ya timu hiyo kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Fadlu, ambaye aliwahi kuiongoza Simba kabla ya kuondoka, alikuwa akitajwa kuwa miongoni mwa makocha waliokuwa kwenye orodha ya Yanga katika harakati za kumpata mrithi wa benchi la ufundi kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Baada ya mazungumzo hayo kuvunjika, Yanga sasa imeelekeza nguvu zake kwenye chaguo jingine la makocha, huku uongozi ukiendelea na mchakato wa kumpata kocha mkuu atakayekuwa sehemu ya maandalizi ya msimu wa 2026/27.
Uamuzi huo unaifanya Yanga kuendelea na mipango yake ya kujenga kikosi imara, huku ikitarajia kupata kocha mwenye uwezo wa kuiongoza timu hiyo kwenye mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.