Yanga Yazidi Kukumbwa Na Vikwazo Katika Usajili Wa Kombo
UONGOZI wa timu TRA United umeingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania saini ya nahodha wao, Nasri Kombo, baada ya kuonyesha nia ya kumbakisha kiungo huyo ambaye amekuwa akihusishwa na uhamisho wa kujiunga na Yanga.
Taarifa zinaeleza kuwa Kombo tayari amefanya mazungumzo chanya na mabingwa hao wa Tanzania, Yanga, katika hatua za awali za mipango ya kuhamia Jangwani, lakini sasa TRA United imeamua kuingilia kati ili kuhakikisha nyota huyo habebi mizigo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, viongozi wa TRA United wamemuita Kombo mezani kwa ajili ya mazungumzo ya hatma yake, huku wakitajwa kuwa tayari kuweka mezani ofa kubwa zaidi ya ile inayodaiwa kutolewa na Yanga.
Kombo ambaye kwa sasa yupo kwenye nafasi ya mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake, amekuwa akivutiwa na klabu kadhaa kutokana na uwezo wake pamoja na uzoefu alioupata akiwa sehemu ya kikosi cha TRA United.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa wiki hii inatarajiwa kuwa muhimu katika kufahamu uamuzi wa mwisho wa Kombo, ikiwa ataendelea kubaki ndani ya TRA United au kuhamia Yanga wa ajili ya changamoto mpya.
Yanga imekuwa ikifuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo katika harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano, lakini sasa inakutana na ushindani kutoka kwa waajiri wake wa zamani.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho utakuwa mikononi mwa Kombo mwenyewe baada ya kusikiliza ofa zote zinazowekwa mezani, huku pande zote zikisubiri majibu ya nahodha huyo katika siku chache zijazo.