Habari za michezo

Uswizi Yatinga Robo Fainali Kwa Matuta, Kobel Ageuka Shujaa

Vardo July 8, 2026 11:50 am

VANCOUVER, CANADA: Kipa Gregor Kobel ameibuka shujaa wa Uswisi baada ya kuiongoza timu hiyo kutinga robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 kwa kuichapa Colombia kwa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia sare tasa ya dakika 120 katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa usiku wa kuamkia leo Jumatano  kwenye Uwanja wa BC Place.

Ushindi huo umeifanya Uswisi kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya tatu pekee katika historia yake na kwa mara ya kwanza tangu ilipofanikisha hilo mwaka 1954 ilipoandaa mashindano hayo.

Sasa itakutana na bingwa mtetezi, Argentina, katika pambano litakaloamua timu ya kutinga nusu fainali.

Mchezo ulianza kwa kasi huku Colombia ikionekana kutawala umiliki wa mpira kupitia viungo wake wakiongozwa na James Rodríguez na Jefferson Lerma, waliomzuia nahodha wa Uswisi, Granit Xhaka kucheza kwa uhuru.

Colombia ilitengeneza nafasi ya kwanza ya hatari kupitia Gustavo Puerta aliyepiga shuti la mbali lililookolewa kwa ustadi na Kobel huku upande wa pili Camilo Vargas naye akifanya kazi kubwa kuzuia mashuti makali ya Fabian Rieder na Dan Ndoye.

Licha ya timu zote kushambuliana mara kwa mara, hakuna iliyoweza kupata bao katika kipindi cha kwanza na kwenda mapumziko zikiwa zimefungana 0-0.

Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa zaidi huku kila timu ikisaka bao la ushindi. Uswisi ilikaribia kupitia Rieder aliyepiga mpira wa adhabu uliopita karibu na lango, wakati Luis Díaz aliendelea kuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya wapinzani.

Dakika 90 zilimalizika bila mshindi na mchezo ukaingia muda wa nyongeza.

Katika dakika za nyongeza Colombia iliamini ilistahili kupewa penalti baada ya mchezaji wake kuangushwa ndani ya eneo la hatari, lakini mwamuzi aliendelea na mchezo.

Baadaye beki, Jhon Lucumí alikaribia kuifungia Colombia kwa kichwa kilichogonga mwamba wa juu wa lango kabla ya kutoka nje.

Uswisi nayo ilijibu mashambulizi kupitia Zeki Amdouni ambaye alimlazimisha Vargas kuokoa. Dakika 120 zilipomalizika bila bao, mshindi aliamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Katika mikwaju hiyo, Colombia ilianza vibaya baada ya Davinson Sánchez kupiga mpira uliogonga mwamba wa juu.

Hata hivyo,  Uswisi ilitoa nafasi hiyo baada ya Manuel Akanji kukosa penalti yake.

Shujaa wa mchezo alikuwa Kobel aliyedaka penalti ya Cucho Hernández na kuipa Uswisi nafasi ya kushinda kabla ya Rubén Vargas kufunga penalti ya mwisho na kuipeleka Uswisi robo fainali kwa ushindi wa penalti 4-3.

Kobel alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi kutokana na kiwango chake bora ndani ya dakika 120 na katika mikwaju ya penalti.

Kwa Colombia, ilikuwa mwisho wa safari ya Kombe la Dunia kwa maumivu huku ikiendelea kuwa na rekodi mbaya dhidi ya timu za Ulaya mwaka huu.

Sasa macho yote yataelekezwa kwenye robo fainali ambapo Uswisi itakabiliana na Argentina, timu iliyofuzu baada ya kuiondoa Misri katika mchezo uliotangulia wa hatua ya 16 bora.

Barabara Za AFCON Mbioni Kukamilika Samatta Aaga Taifa Stars, AFCON 2027 Atabaki Jukwaani