Habari za michezo

Camavinga Kutimkia Man City

Vardo July 8, 2026 1:33 pm

MADRID, Hispania: KIUNGO Eduardo Camavinga ni mmoja wa wachezaji wanaotajwa wanaweza kuondoka Real Madrid CF katika dirisha hili la usajili akitajwa kuelekea Manchester City.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika saa za hivi karibuni kumekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Real Madrid na Manchester City F.C. kuhusu uwezekano wa uhamisho wa kiungo huyo wa Ufaransa.

Hatua hiyo inadaiwa kuungwa mkono na kocha Jose Mourinho, ambaye anaripotiwa kutoridhishwa na kiwango alichoonyesha Camavinga katika misimu ya hivi karibuni akiwa Real Madrid.

Inadaiwa Manchester City imepokea pendekezo kutoka Real Madrid na kwa sasa inalitathmini. Camavinga anaonekana kuwa na sifa nzuri ndani ya kikosi cha miamba hiyo ya England kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii, nguvu za mwili na uchezaji wa katikati ya uwanja.

Katika dirisha hili la usajili, City tayari imemsajili kiungo wa kimataifa wa England, Elliot Anderson, kwa ada inayodaiwa kufikia euro135 milioni. Aidha, klabu hiyo ilikuwa pia ikimfuatilia Sandro Tonali, lakini taarifa zinaeleza kuwa Tottenham Hotspur ndiyo inayotarajiwa kukamilisha usajili wake kwa zaidi ya euro100 milioni kutoka Newcastle United.

Kutokana na hali hiyo, Real Madrid inaona uwezekano wa kumuuza Camavinga kama fursa nzuri ya kibiashara, hasa ikizingatiwa kuwa Manchester City bado inahitaji kuimarisha safu ya kiungo pia uwezo wake mkubwa wa kifedha.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Mourinho anaamini Real Madrid bado inahitaji kuongeza wachezaji wawili zaidi mmoja wa kiungo na mwingine wa beki wa kati hivyo fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya Camavinga zinaweza kusaidia kufanikisha usajili huo.

Wakati huohuo, Manchester City imekuwa ikifanya kazi pia kumsajili chipukizi wa Morocco, Ayyoub Bouaddi, kutoka Lille OSC.

Inadaiwa mazungumzo kati ya pande hizo tayari yamefanyika, huku City ikitafakari kama imsajili mara moja au imuache kwa mkopo Lille kwa msimu mmoja zaidi.

Hadi sasa, Real Madrid imewaaga wachezaji watatu ikilinganishwa na kikosi cha msimu uliopita. Dani Carvajal na David Alaba waliondoka baada ya mikataba yao kumalizika, huku klabu hiyo pia ikimruhusu Dani Ceballos kuondoka bure na sasa yuko huru kujadili mustakabali wake.

Mbali na hao, kuna uwezekano wa wachezaji wengine kuondoka, huku Fran Garcia na Raul Asencio wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kuondoka.

Samatta Aaga Taifa Stars, AFCON 2027 Atabaki Jukwaani Arbeloa Aula Fulham