Simba SC

Hatma Ya Maema Yawagawa Barker Na Viongozi Simba

Vardo July 9, 2026 10:27 am

WAKATI hatma ya kiungo Neo Maema ndani ya Simba ikiendelea kuwa gumzo, kocha mkuu Steve Barker ameibua mjadala mpya baada ya kuonyesha wazi kuwa bado anahitaji huduma ya nyota huyo katika kikosi chake kwa msimu wa 2026/27.

Taarifa zinaeleza kuwa Barker amewapa kazi ngumu viongozi wa Simba kwa kusisitiza kuwa Maema anapaswa kupewa mkataba mpya baada ya ule wa mkopo kumalizika, akiamini bado ana mchango mkubwa ndani ya kikosi.

Kauli ya hivi karibuni ya Maema pia imezidi kuongeza mjadala baada ya kuweka wazi kuwa hajafunga mlango wa kuendelea kubaki Simba, akisema kuwa “chochote kinawezekana” kuhusu mustakabali wake.

Inaelezwa kuwa Barker alianza kuonyesha imani yake kwa Maema tangu alipompa nafasi katika mechi muhimu, ikiwemo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB. Hatua hiyo ilitafsiriwa na wengi kuwa ishara ya jinsi kocha huyo anavyouthamini mchango wa kiungo huyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, Barker anaamini Maema alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika mfumo wake msimu uliopita, akichangia mafanikio yaliyoisaidia Simba kutwaa mataji mawili ya ndani na kufikia malengo yake ya msimu.

“Barker amewaeleza viongozi kuwa anahitaji Maema aendelee kubaki kikosini na amependekeza apewe mkataba mpya baada ya ule wa mkopo kumalizika. Hata hivyo, viongozi bado wanatafakari kuhusu hatma yake,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa baada ya kumalizika kwa msimu, viongozi wa Simba walifanya tathmini ya kikosi na kufikia uamuzi wa kutafuta kiungo mwingine wanayeamini ataongeza ushindani na ubora zaidi eneo la kiungo.

Tofauti hiyo ya mtazamo kati ya benchi la ufundi na uongozi imeendelea kuibua maswali kuhusu mustakabali wa Maema, huku maamuzi ya mwisho yakisubiri kukamilika kwa mazungumzo yanayoendelea.

Chanzo hicho kimeongeza kuwa uamuzi rasmi kuhusu hatma ya Maema unatarajiwa kutolewa katika siku zijazo, hatua ambayo itaondoa sintofahamu kuhusu kama kiungo huyo ataendelea kuitumikia Simba au atatafuta changamoto mpya.

Superkompyuta Yatabiri England Kutolewa Na Argentina Messi Kubeba Tena Kombe La Dunia Yanga Waanze Kujipanga, Beki Simba Aeleza Nguvu Mpya Msimu Ujao