Simba SC

Yanga Waanze Kujipanga, Beki Simba Aeleza Nguvu Mpya Msimu Ujao

Vardo July 9, 2026 10:33 am

BEKI wa Simba SC, Rushein De Reuk, ametuma ujumbe mzito kwa wapinzani wao kuelekea msimu wa 2026/27 akisema mafanikio ya kutwaa mataji mawili msimu uliopita yameongeza nguvu, kujiamini na kiu ya ushindani ndani ya kikosi hicho.

Simba ilimaliza msimu wa 2025/26 ikiwa na furaha baada ya kutwaa Kombe la Muungano pamoja na Kombe la CRDB Federation Cup, mafanikio ambayo De Reuk anaamini yamekuwa chachu kubwa kwa timu hiyo kuendelea kupambana na kutafuta makubwa zaidi msimu ujao.

beki huyo raia wa Afrika Kusini amesema wachezaji kwa sasa wanatumia muda wa mapumziko kabla ya kurejea kwenye maandalizi mapya huku wakiwa na kiu kubwa ya ushindani na mafanikio zaidi.

De Reuk amesema anajivunia kuwa sehemu ya kikosi kilichofanikiwa kushinda mataji hayo mawili, huku akieleza furaha yake baada ya kuaminiwa kuwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo kwa kupewa nafasi ya kuvaa kitambaa cha unahodha.

“Msimu unapofikia tamati, ninajisikia fahari kubwa kuwa nimepewa nafasi ya kuiongoza timu hii kubwa kama nahodha. Kushinda mataji mawili pamoja ni jambo ambalo tutalithamini daima, na ni zawadi ya kazi kubwa, kujituma na imani tuliyoonyesha katika msimu mzima,” amesema De Reuk.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamewapa morali zaidi kuelekea msimu mpya, ambapo lengo lao ni kuendelea kupigania mataji waliyoshinda pamoja na kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbali na hilo, De Reuk alitoa pongezi kwa mashabiki wa Simba kwa namna walivyokuwa nyuma ya timu katika kipindi chote cha msimu, akisema sapoti yao iliipa timu nguvu ya kusimama imara wakati wa ushindi na changamoto.

“Shukrani kubwa kwa mashabiki wetu wa ajabu. Msaada wenu usioyumba katika kila hatua, wakati wa mafanikio na changamoto, ulitupa nguvu ya kuendelea kupambana. Haikuwa safari rahisi, lakini kuwa nanyi nyuma yetu kulifanya tofauti kubwa,” ameongeza.

Kwa sasa, Simba inaelekeza nguvu zake kwenye maandalizi ya msimu mpya huku ikitarajia kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kushindania mataji ya ndani na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Hatma Ya Maema Yawagawa Barker Na Viongozi Simba