Simba SC Yatuma Onyo La Usajili 2026/27:”Hatuundi Timu, Tunaongeza Barafu”
Baada ya kufanya maboresho makubwa kwenye kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27, Simba SC imeendelea kutuma ishara nzito ya dhamira yake ya kurejea kileleni mwa soka la Bongo. Safari hii, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa wapinzani wao wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kwa ajili ya ushindani mkubwa ujao.
Ahmed amebainisha kuwa Wekundu wa Msimbazi hawapo tena kwenye hatua au mpango wa “kujenga upya” kikosi. Badala yake, mkakati wa sasa ni kufanya maboresho ya kimkakati kwa kuongeza wachezaji wenye ubora wa juu ambao wataingia kuongeza nguvu kwenye timu thabiti iliyopo tayari.
Akifafanua zaidi kuhusu dira na mipango ya usajili ya Simba SC, Ahmed alieleza kuwa ingizo jipya la wachezaji haliji kuanza sifuri, bali kuongeza thamani na kuchochea ushindani wa namba ndani ya kikosi ambacho tayari kina msingi imara.
“Safari hii hatufanyi usajili wa kubahatisha, tunaongeza wachezaji bora kwenye timu yetu bora. Ni kama vile kuweka barafu kwenye kinywaji kitamu au kurembea sukari ya barafu (ice sugar) kwenye keki ya birthday,” alisema Ahmed Ally kwa kujiamini.
Kauli hii ya kijamii inakuja wakati Simba SC ikikamilisha hatua za mwisho za kusuka kikosi chake, huku malengo makuu yakiwa ni kurejesha heshima ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) na kufika mbali zaidi kwenye michuano mikubwa ya kimataifa.
Katika dirisha hili la usajili, Simba imethibitisha kuwa miongoni mwa klabu zinazotikisa sokoni, huku viongozi wakisisitiza kuwa lengo ni kuwa na kikosi kipana chenye ushindani wa hali ya juu katika kila idara. Kwa ujumbe huu mzito, Ahmed Ally anaamini kuwa msingi wa Wekundu wa Msimbazi umeshakamilika, na kilichobaki sasa ni kuwasha moto wa burudani na ushindi msimu ujao.