Sare za Simba CECAFA Kagame Cup
Simba SC

Sare za Simba CECAFA: Patrick Rweyemamu Afunguka Maandalizi ya Msimu Mpya

Vardo July 29, 2026 7:02 pm

Uongozi wa klabu ya Simba SC umewataka mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi wowote kufuatia matokeo ya sare mbili mfululizo katika michuano ya CECAFA Kagame Cup, ukisisitiza kuwa matokeo hayo sio kipimo halisi cha ubora wa kikosi chao.

Simba imelazimishwa sare za bila kufungana () dhidi ya Mogadishu City Club (MCC) pamoja na Jamus FC, matokeo yaliyozua mijadala mbalimbali miongoni mwa wapenzi wa soka. Hata hivyo, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, amebainisha kuwa kikosi kipo kwenye mwelekeo sahihi wa maandalizi ya msimu mpya wa 2026/27.

CECAFA Kama Sehemu ya Pre-Season

Akizungumzia hali ya kikosi, Rweyemamu alieleza kuwa ratiba iliyo mbele yao ni ngumu na yenye presha kubwa, hivyo benchi la fundi limeamua kutumia ushindani wa Kagame Cup kujenga utimamu wa wachezaji.

“Presha ya hizi mechi ni kubwa sana. Tuko CECAFA, lakini pia tunajiandaa kwa mechi za maandalizi, tamasha la Simba Day, mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, na baadaye mechi yetu ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar. Hivyo tunaitumia CECAFA kama sehemu ya pre-season wetu,” amesema Rweyemamu.

Ameongeza kuwa tofauti na mazoea ya kucheza mechi za kirafiki pekee, safari hii Simba imeamua kutumia mashindano haya ili kuwapa wachezaji nafasi ya kuzoeana katika mazingira ya ushindani wa kweli.

Utimamu wa Miili na Muunganiko wa Timu

Rweyemamu pia amebainisha kuwa baadhi ya timu wanazokutana nazo katika michuano hiyo zilianza maandalizi mapema, jambo linalozifanya ziwe mbele kidogo kiutimamu, huku Simba ikiendelea kujenga muunganiko wa kikosi chake kipya.  

“Baadhi ya timu tunazokutana nazo tayari zimemaliza pre-season zao, lakini sisi tunaitumia CECAFA kujenga timu na kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya,” alihitimisha Rweyemamu.  

Meridianbet Yatoa Mwangaza Kwa Kaya Mbalimbali Buguruni Kurejea kwa Neo Maema Simba Kwawapa Presha Wawili Hawa Msimbazi!