Mchezaji Chipukizi Morocco Afariki Dunia Akijaribu Kuvuka Bahari Kuelekea Ulaya
MAISHA yanatafutwa kwa jasho na damu, na mara nyingi safari ya kuelekea mafanikio hubeba hatari kubwa—hadi kuweka rehani uhai.
Ulimwengu wa soka nchini Morocco umeingia kwenye huzuni kubwa kufuatia kifo cha ghafla cha mwanasoka chipukizi mwenye umri wa miaka 20, Faten Ben Amar El Aziz, aliyefariki dunia akijaribu kuvuka bahari kuelekea eneo la Ceuta linalotawaliwa na Hispania.
Faten, aliyekuwa akiipigania nembo ya klabu ya Maghreb Athlétique Tétouan nchini Morocco, alikuwa na kiu ya kubadilisha maisha yake na ya familia yake kupitia kipaji chake cha kusakata kabumbu. Ndoto yake kubwa ilikuwa kufika barani Ulaya kujiunga na akademi au klabu yoyote ili kufuata nyayo za nyota wa kimataifa wa Morocco kama Achraf Hakimi (PSG) na Brahim Diaz (Real Madrid).
Safari ya Hatari Iliyoishia Simanzi
Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Morocco, kijana huyo alikuwa miongoni mwa kundi la watu waliotaka kuingia Ceuta—eneo la Hispania lililopo pwani ya Afrika Kaskazini linalopakana na Morocco.
Katika jaribio hilo, Faten alilazimika kuogelea kupitia eneo la bahari la Tarajal, ambalo linajulikana kwa hatari yake kutokana na mawimbi makali na ulinzi mkali wa mipakani. Kwa bahati mbaya, safari hiyo ya kusaka maisha bora iligeuka kuwa mauti baada ya kuzama baharini na kukatiza ghafla ndoto zake zote.
Kifo cha Faten kimeacha majeraha makubwa na huzuni isiyoaminika kwa familia yake, wachezaji wenzake katika klabu ya Tétouan, pamoja na mashabiki wa soka kote nchini Morocco na Afrika kwa ujumla. Kisa hiki kinaendelea kuonyesha taswira halisi ya changamoto na hatari wanazopitia vijana wengi wa Afrika wanaojaribu kutafuta fursa za maisha barani Ulaya.