Rasmi: Simba SC Yaikimbia Uhuru, Yarejea Meja Isamuhyo Dhidi ya Coastal Union (+Viingilio na Tiketi)
KLABU ya Simba imeamua kuachana na Uwanja wa Uhuru na kurejea kutumia Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo kwa mechi zake za nyumbani katika mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Hatua hiyo imetangazwa na uongozi wa Simba, ukisema Uwanja wa Meja Isamuhyo ndio utatumika kama uwanja wa nyumbani wa timu hiyo kuanzia mchezo dhidi ya Wagosi wa Kaya utakaochezwa Agosti 27, mwaka huu.
Simba awali ilianza kutumia Uwanja wa Uhuru kama kituo chake cha nyumbani, lakini sasa imeamua kurejea Meja Isamuhyo, uwanja ambao ilitumia msimu uliopita na kufanikiwa kufanya vizuri bila kupoteza mchezo hata mmoja.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewashukuru viongozi na wadau wa Uwanja wa Meja Isamuhyo kwa kuiruhusu klabu hiyo kurejea kutumia dimba hilo.
Ally amesema Simba imechagua Meja Isamuhyo kutokana na kumbukumbu nzuri za msimu uliopita, huku akiamini uwepo wa mashabiki wengi utakuwa sehemu muhimu ya kuipa timu nguvu katika mechi za nyumbani.
“Uwanja ambao tulitumia vyema msimu uliopita, ni ngome yetu ya ushindi na kwa mantiki hiyo turejee tena katika uwanja huu,” amesema Ally.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni mfumo mpya wa ununuzi wa tiketi kwa njia ya simu, ambao unatarajiwa kutumika katika mechi hizo.
Amesema mchezo wa Agosti 27 utakuwa miongoni mwa mechi za kwanza ambazo mashabiki wengi wa Simba watakutana na mfumo huo mpya wa tiketi, hivyo amewataka kujiandaa mapema.
“Ni mfumo mpya, rahisi kununua tiketi lakini sababu ni mpya. Mfumo huu hautaji kwenda kituoni kununua tiketi kama ilivyokuwa hapo awali, unaweza kununua kwa simu,” amesema.
Kwa upande wa viingilio, Ally amesema Simba imeweka Sh5,000 kwa mashabiki watakaokaa sehemu za Mzunguko, huku tiketi ya VIP ikiwa Sh10,000.
Amesema licha ya Uwanja wa Meja Isamuhyo kuwa mdogo ukilinganisha na baadhi ya viwanja, Simba inaamini hautakuwa na changamoto kubwa kwa mashabiki wake.
“Msimu uliopita tulicheza kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo na hatukupoteza mchezo hata mmoja. Ni sehemu salama kweli kweli kwa upande wetu,” amesema.
Wakati huo huo, Ally amesema kikosi cha Simba kilirejea jana kutoka Singida na leo kimeanza maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Wagosi wa Kaya.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na mwanzo mzuri wa msimu baada ya kukusanya pointi sita katika michezo yake miwili ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara.