Mngqithi Amfunda Risasi Chuga Boy: Yanga Yapiga 4-1 JKT Tanzania | Soka La Bongo
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, amemjia juu mshambuliaji wake chipukizi, Issa Bushiri ‘Chuga Boy’, na kumtaka kuachana mara moja na tabia ya kucheza kwa ubinafsi, badala yake aweke maslahi ya timu mbele.
Kauli hiyo ya Mngqithi imekuja mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, ambapo Yanga iliondoka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Tanzania.
Licha ya ushindi huo mkubwa, Mngqithi hakufurahishwa na kiwango cha Chuga Boy na kumtaka mchezaji huyo kujitathmini kwa kina ili kubadilika, ingawa alikiri kuwa kijana huyo ana kipaji kikubwa kinachoweza kumfikisha mbali.
“Chuga Boy hakufanya vizuri na sikufurahishwa naye kwa sababu alikuwa akicheza kwa ajili yake mwenyewe. Anatakiwa kujirekebisha kwa sababu timu ni kubwa kuliko mtu mmoja. Sitaki wachezaji wanaocheza kwa ajili yao, nataka wanaocheza kwa ajili ya timu,” alisema Mngqithi.
Hata hivyo, Mngqithi alibainisha kuwa bado ana imani kubwa na uwezo wa mchezaji huyo na yupo tayari kumlea na kumfunda ili akue kisoka, akisisitiza kuwa umri wake mdogo unampa nafasi kubwa ya kuwa mchezaji hatari zaidi nchini.
“Ni kijana mdogo na tunapaswa kumuunga mkono, kufanya naye kazi na kuhakikisha anaimarika kwa sababu ana kipaji kikubwa sana. Lakini hapaswi kuwa mbinafsi. Akiwa mnyenyekevu na kucheza kwa ajili ya timu, atakua kwa urahisi, lakini akitaka kufanya mambo yake mwenyewe atajiharibu. Nitaongea naye,” aliongeza.
Sure Boy Amkosesha Mngqithi Maneno
Wakati akiwa mkali kwa Chuga Boy, Mngqithi hakuwa nyuma kumwagia sifa kedekede kiungo mzoefu wa timu hiyo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kwa namna alivyotekeleza maelekezo yake kikamilifu na kutawala eneo la katikati ya uwanja.
Kocha huyo alisema alimtaka Sure Boy kucheza kwa utulivu na kupunguza presha uwanjani, jambo ambalo kiungo huyo alilinyanyua na kulitekeleza kwa asilimia mia moja.
“Nimefurahishwa sana naye. Nilimtaka atawale mchezo, acheze kwa urahisi, asijipe presha na kuhakikisha timu inaendelea kwenda mbele. Alicheza kulingana na maelekezo exact,” alisema Mngqithi.
Kocha huyo aliongeza kuwa nidhamu ya Sure Boy katika upigaji wa pasi sahihi ndiyo siri ya yeye kujihakikishia namba kwenye kikosi chake cha kwanza:
“Unaweza kuona ni mchezaji bora, ni gwiji wa timu hii. Nilifurahishwa sana na namna alivyofuata maelekezo. Sidhani kama alipoteza hata mpira mmoja. Kwangu mimi, ukiwa na kiwango kizuri cha ukamilishaji wa pasi, unajihakikishia nafasi ya kucheza kwenye timu yangu.”
Mngqithi alitimisha kwa kusema kuwa benchi la ufundi linaendelea kupambana kujenga kikosi imara na chenye ushindani, na kwamba kila mchezaji anapaswa kutambua wajibu wake ili kufikia malengo ya klabu hiyo msimu huu.