Sakata la Mtoto wa Miaka 11: Jux Avunja Ukimya, Aweka Sauti ya Simu Wazi Dhidi ya Happy
Sakata linalomhusisha msanii wa Bongo Fleva, Juma Jux, na mwanamke anayetambulika kwa jina la Happy, limechukua sura mpya baada ya pande zote mbili kutoa kauli zinazokinzana vikali kuhusu madai ya mtoto mwenye umri wa miaka 11.
Jux, ambaye ni mume wa Priscilla Ojo (binti wa mwigizaji mkongwe wa Nollywood, Iyabo Ojo) na baba wa mtoto mmoja aliyezaliwa Canada Agosti 2025, amejikuta katikati ya mjadala mzito mitandaoni.
Madai ya Happy na Ombi la DNA Happy ndiye aliyeibua mtimanyongo huo akidai kuwa Jux ni baba mzazi wa mtoto wake na kwamba amekuwa akitenga majukumu ya malezi. Baada ya madai hayo kusambaa, Happy alionekana kwenye video akimwomba msaada Waziri mwenye dhamana ya wanawake na watoto ili amsaidie kupata kipimo cha DNA, akisisitiza ndicho kitakachoweka ukweli wazi.
Uongozi wa African Boy na Jux Wakanusha Upande wa Jux kupitia lebo yake ya African Boy umepinga vikali taarifa hizo na kuzitaja kuwa za kutungwa, ukisisitiza kuwa Jux na Happy hawajawahi hata kukutana.
Akizungumzia swala hilo, Jux alieleza kuwa mwanzo aliamua kukaa kimya lakini amelazimika kuzungumza baada ya suala hilo kuanza kuchafua jina lake, familia yake na biashara zake.
“Mhusika alithibitisha kwa maneno na sauti yake kuwa hakuwahi kukutana kimwili na mimi wala kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mimi… Kwa upande wangu, nimechagua utulivu, ukweli na hatua sahihi za kisheria,” alieleza Jux.
Ushahidi wa Sauti Waibua Mapya Kudhihirisha msimamo wao, uongozi wa African Boy HQ umeachia kanda ya sauti inayodaiwa kuwa ni mazungumzo ya simu kati ya Jux na Happy. Katika sauti hiyo, mwanamke anayesikika anakiri kuwa mtoto huyo si wa Jux—jambo linalokinzana kabisa na kauli za awali za Happy za kutaka kipimo cha DNA.