Ronaldo na Messi Kucheza Timu Moja? Carlos Tevez Aandaa Mchezo wa Aina Yake La Bombonera
BUENOS AIRES, ARGENTINA — Mastaa wawili wakubwa wa soka duniani katika kizazi hiki, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, wanatarajiwa kuandika historia mpya kwa kucheza timu moja kwa mara ya kwanza kabisa mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa zaidi ya miongo miwili, ulimwengu wa soka umeshuhudia ushindani mkali na wa kuvutia kati ya miamba hii wawili. Wakiwa wamekutana mara 37 katika ngazi ya klabu na timu za taifa, wawili hawa wameacha alama isiyofutika kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Mchezo wa Kumuaga Carlos Tevez
Ripoti kutoka nchini Argentina zinasimulia kuwa wawili hao wanaweza kuungana kupitia mchezo maalum wa kumuaga aliyekuwa mchezaji mwenzao, Carlos Tevez.
Tevez (42), ambaye alitangaza kustaafu soka mwaka 2021 akiwa na klabu yake ya utotoni ya Boca Juniors, anapanga kutumia uwanja wa La Bombonera wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 57,000 kufanya tukio hilo kubwa linalotarajiwa kufanyika mwezi Desemba.
Mipango ya Tevez Kutimiza Ndoto ya Mashabiki
Tevez anapanga kualika takribani wachezaji 60 aliowahi kucheza nao pamoja na marafiki zake wa karibu. Mipango hiyo inajumuisha kuunda vikosi viwili:
-
Kikosi cha Marafiki wa Karibu: Kitakachoundwa na wachezaji wa karibu zaidi na Tevez.
-
Kikosi cha Wachezaji Wenzake wa Zamani: Kitakachojumuisha nyota aliocheza nao katika klabu mbalimbali.
Tevez aliwahi kucheza na Messi katika timu ya taifa ya Argentina, huku akiwa mchezaji mwenza wa Ronaldo kwa misimu miwili ndani ya Manchester United.
Akiweka wazi nia yake ya kuwaleta wachezaji hao, Tevez alisema:
“Leo Messi na Cristiano Ronaldo watakuwepo. Ikiwa itabidi niende kuwachukua mwenyewe, nitafanya hivyo. Nina namba zao wote kwenye WhatsApp.”
Mastaa Wengine Wanaotarajiwa Kualikwa
Rais wa Boca Juniors, Juan Roman Riquelme, amempa baraka zote Tevez kufanya tukio hilo katika uwanja wa La Bombonera. Mbali na Messi na Ronaldo, nyota wengine wanaotajwa kualikwa ni:
-
Wayne Rooney
-
Rio Ferdinand
-
Andrea Pirlo
-
Gianluigi Buffon
Takwimu za Tevez Akiwa na Messi na Ronaldo
Tevez na Lionel Messi:
-
Mechi walizocheza pamoja: 47
-
Assist za Messi kwa Tevez: 6
-
Assist za Tevez kwa Messi: 4
Tevez na Cristiano Ronaldo:
-
Mechi walizocheza pamoja: 80
-
Assist za Tevez kwa Ronaldo: 4
-
Assist za Ronaldo kwa Tevez: 5