RUSHEIN AIBUA ‘SILAHA’ NZITO YA SIMBA KUIANGAMIZA MIGHTY WANDERERS BENJAMIN MKAPA
NAHODHA wa Simba SC, Rushein De Reuck, amefichua kuwa ushindi wa ugenini na nidhamu ya kulinda lango (clean sheet) ndiyo ‘silaha’ kuu itakayoibeba timu hiyo kuisambaratisha Mighty Wanderers ya Malawi kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba iliondoka na ushindi muhimu wa bao 1-0 ugenini nchini Malawi katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali. Mchezo wa marudiano unatarajiwa kupigwa Septemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam.
De Reuck ameweka wazi kuwa ingawa mechi ya kwanza ilikuwa ngumu kutokana na upinzani mkali wa Wanderers, wachezaji walipambana kwa jasho na damu kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi na kutoruhusu bao.
Mbinu Mpya ya Marudiano Dar es Salaam
Akizungumzia mchezo wa marudiano, nahodha huyo amesisitiza kuwa sura ya mchezo itabadilika kabisa pindi watakapokuwa nyumbani mbele ya mashabiki wao.
“Tulijua kucheza ugenini ingekuwa vigumu kwa sababu Mighty Wanderers ni timu nzuri. Tuliteseka kidogo lakini haya ndiyo mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na lazima uwe tayari kwa kila hali,” alisema De Reuck.
Ameongeza kuwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba imepanga kutawala mpira mwanzo hadi mwisho na kutumia kikamilifu nafasi zitakazotengenezwa ili kupata mabao ya kutosha.
“Tutacheza nyumbani wiki hii, hivyo tunahitaji kuudhibiti mchezo kwa zaidi ya asilimia 100. Tunataka kucheza kama timu kubwa, kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao. Lengo letu ni kushinda kwa kishindo na kusonga mbele kwa kujiamini,” aliongeza De Reuck.