Steve Barker Simba SC
Simba SC

Barker Afichua Siri ya Ushindi wa Simba Malawi, Atoa Tamko Zito Marudiano Dar

Vardo September 7, 2026 5:56 pm

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amewasifu wachezaji wake kwa kuonyesha uimara na uvumilivu mkubwa uliowawezesha kuondoka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, katika mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ilipata ushindi huo muhimu kupitia bao la mshambuliaji Anicet Oura—matokeo yanayoipa faida kubwa kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 12, 2026, jijini Dar es Salaam.

Barker Aeleza Ugumu wa Mchezo na Uwanja

Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker alikiri kuwa mechi haikuwa rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao pamoja na hali ya uwanja.

“Ulikuwa mchezo mgumu sana. Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa, lazima uthamini ushindani unaokutana nao ugenini. Mighty Wanderers walikuwa na hamasa kubwa, lakini wachezaji wangu walionyesha uimara na kuvumilia nyakati ngumu,” alisema Barker.

Siri ya Bao la Anicet Oura

Akimzungumzia mfungaji wa bao hilo, Barker alisema lilipatikana kutokana na umakini wa Oura kutumia makosa ya safu ya ulinzi ya wapinzani.

“Ni nadra kuona mabao ya aina hiyo. Beki wao hakuwa na uhakika, na bahati nzuri Anicet alikuwa mwepesi kusoma upepo na kuwahi mpira. Kwenye mechi ngumu kama hizi, unahitaji fursa kama hizo kufanya tofauti,” aliongeza kocha huyo.

Rai Mzito kwa Mashabiki wa Simba

Barker hakusahau kutoa shukrani kwa mashabiki waliosafiri hadi Malawi kuipa timu nguvu, huku akiwaomba kujitokeza kwa wingi zaidi katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.

“Ni jambo la kushangaza na la kupongezwa kuona mashabiki wengi kiasi hiki ugenini. Tunawashukuru sana. Sasa tunaihitaji sapoti hiyo zaidi nyumbani wiki ijayo; tunatamani kuona uwanja ukijaa ili utupe nguvu ya kutinga hatua inayofuata,” alihitimisha.

Mighty Wanderers vs Simba SC: Kocha Mabedi Kurudisha Mapigo Dar