Selemani Mwalimu Atamani Uchezaji Bora Yanga vs Gaborone United
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Selemani Mwalimu, amesema anatamani kuibuka mchezaji bora katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, huku akisisitiza kuwa jukumu lake ni kuendelea kutoa kiwango bora kwa ajili ya timu.
Mwalimu amesema anafurahia nafasi aliyopewa na benchi la ufundi na kwamba kufanya majukumu yake kwa umakini ndiyo sababu ya kupata kiwango kizuri uwanjani. Amesema pamoja na kutamani kutwaa tuzo hiyo, jambo la msingi kwake ni kuhakikisha anaendelea kuisaidia timu kupata matokeo inayoyahitaji.
“Napenda nichukue mchezaji bora wa mechi dhidi ya Gaborone. Ningependa kuwa shujaa katika mchezo huo, lakini kubwa ni kushika majukumu yangu vizuri ili niweze kupata performance nzuri,” amesema Mwalimu.
Mbali na hilo, mshambuliaji huyo ameuelezea furaha yake kutokana na uongozi wa Yanga kumpa siku maalumu ya kumuenzi, akisema ni heshima kubwa ambayo ameipokea kutoka kwa klabu hiyo na ambayo hajawahi kuiona kwa kiwango hicho katika timu nyingine alizowahi kucheza.
Amesema heshima hiyo imempa faraja na kumfanya ajisikie mwenye thamani zaidi ndani ya klabu, huku akitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa Yanga kwa kutambua mchango wake na kumpa siku hiyo maalumu.
“Ninajisikia furaha kwa timu kunipa siku yangu maalumu. Ni faraja na heshima ambayo timu imenipa. Sidhani kama nimewahi kupata heshima kama hii katika timu nyingine,” amesema.
Akizungumzia mchezo wa marudiano dhidi ya Gaborone United, Mwalimu amesema wachezaji wote wana morali kubwa na wamejipanga kuhakikisha wanafikia malengo ya Yanga, akisisitiza kuwa ukubwa wa kikosi unawapa nafasi ya kila mchezaji kupambana kwa ajili ya timu.
Amesema ushindani uliopo ndani ya kikosi haupaswi kugawanya wachezaji, bali unatakiwa kuwafanya kila mmoja kuongeza juhudi na kuhakikisha anapopata nafasi anaitumia vizuri kwa manufaa ya timu.
“Wachezaji tuna njaa kubwa. Malengo yetu ni kufika mbali zaidi. Tuna kikosi kikubwa na kila mchezaji ataipambania timu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema.
Mwalimu amehitimisha kwa kutoa wito kwa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo, akisema uwepo wao uwanjani ni sehemu muhimu ya kuwapa nguvu wachezaji wanapokuwa wakisaka ushindi na nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
“Ni mechi muhimu sana na tunawakaribisha mashabiki waje kwa wingi kusupport timu. Support yenu ndiyo nguvu yetu, hasa tunapocheza nyumbani,” amesema.