Kocha Gaborone United Yanga
Yanga SC

Kocha Gaborone United Afunguka Kasi ya Yanga: “Kipindi cha Kwanza Kilituvuruga”

Vardo September 13, 2026 8:41 am

Kocha Mkuu wa Gaborone United ya Botswana, Sean Connor, amekiri kuwa kasi kubwa iliyoonyeshwa na Yanga SC katika dakika 15 za mwanzo za mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika iliwapa presha kubwa wachezaji wake na kuwafanya kushindwa kucheza kwa utulivu.

Yanga iliibuka na ushindi katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Connor ameeleza kuwa ingawa timu yake ilianza kwa kusuasua kipindi cha kwanza, walirejea kwa kiwango bora zaidi baada ya mapumziko.

Yanga Yaingia na Kasi, Yaweka Presha Kati

Connor alisema Yanga walitawala eneo la kiungo mapema, jambo lililowazuia wageni kumiliki mpira na kutekeleza mpango wao wa kushambulia kupitia maeneo ya pembeni.

“Katika dakika 15 za mwanzo waliingia kwa kasi sana na hatukuweza kukabiliana nayo vizuri. Walitawala mpira kwa muda mrefu, japo sikufikiri kama walitengeneza nafasi nyingi za wazi kipindi hicho,” alisema Connor.

Aliongeza kuwa changamoto kubwa kwa kikosi chake ilikuwa kushindwa kuutuliza mpira chini kipindi cha kwanza, tofauti na nidhamu ya mchezo waliyoonyesha baada ya mapumziko.

Mabadiliko ya Mfumo Yapelekea Uhai Kipindi cha Pili

Kocha huyo alieleza kutoridhishwa na utofauti wa viwango kati ya vipindi viwili, akisisitiza kuwa Gaborone United ina uwezo mkubwa wa kumiliki mchezo.

Katika kipindi cha pili, alifanya marekebisho ya kiufundi kwa kuongeza kiungo mmoja katikati ya uwanja ili kupata udhibiti wa mchezo.

“Kipindi cha pili tuliongeza mtu mmoja katikati. Mwanzo tulijaribu kushambulia kupitia pembeni ili kuingia nyuma ya mabeki wao wa pembeni, lakini haikufanya kazi kama tulivyotarajia,” alifafanua.

Kusaka Bao la Mapema na Tumaini la Baadaye

Connor alibainisha kuwa aliwataka wachezaji wake kuingia kipindi cha pili wakiwa na malengo ya kusaka bao huku wakilinda lango lao.

“Tuliwaambia tuna dakika 45 za kupambana. Lazima tuhakikishe haturuhusu bao jingine na tukipata goli moja tutarejea kwenye mchezo. Tungepata bao mapema, picha ya mchezo ingekuwa tofauti kabisa,” alisema.

Pamoja na matokeo hayo, Connor anaamini timu yake imeondoka na mafunzo muhimu, akisisitiza kuwa tofauti ya nafasi zilizotengenezwa na timu zote mbili haikuwa kubwa kulingana na matokeo ya mwisho ya mchezo.

Mngqithi Aiponda Yanga Baada ya Ushindi dhidi ya Gaborone Utd: “Tungeshinda 7-0” Cheikh Ibrahima Touré: Sina Presha Yanga, Mabao Yatakuja Hivi Karibuni