Ngorongoro Heroes Yaanza Kutetea Ubingwa CECAFA U-20 Dhidi ya Rwanda
TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, leo inaanza rasmi safari ya kutetea ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-20) kwa kuvaana na Rwanda kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa Kundi A utapigwa majira ya saa 2:00 usiku, ambapo Tanzania inalenga kuanza kwa kutoa burudani na ushindi mnono mbele ya mashabiki wa nyumbani. Kundi hilo pia linaijumuisha timu ya taifa ya Ethiopia.
Njia Ya Kuelekea AFCON U-20 Mashindano ya mwaka huu yanashirikisha timu tisa zinazowania nafasi mbili pekee za kuwakilisha ukanda wa CECAFA kwenye Fainali za AFCON U-20 zitakazofanyika mwakani nchini Ghana.
Tanzania inaingia uwanjani ikiwa na shinikizo kubwa la kutetea taji hilo, kufuatia ushindi wao wa mwaka 2024 ambapo waliichapa Kenya 2-1 kwenye mechi ya fainali.
Arafat Ally Azungumzia Presha Na Maandalizi Akizungumza kuelekea pambano hilo, Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Arafat Ally—ambaye anakipiga katika klabu ya ENNPI inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri—amewatoa hofu Watanzania na kueleza kuwa kikosi kiko tayari.
“Tunashukuru Mungu tuko salama. CECAFA ni mashindano makubwa yanayokutanisha timu bora za ukanda huu, hivyo kwetu wachezaji ni jukwaa zuri la kuonyesha vipaji vyetu. Tunajua Rwanda ni timu ngumu na yenye ubora, lakini mbinu tulizopewa na kocha wetu tutazitumia kikamilifu kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu,” amesema Arafat.
Ratiba Ya Mechi Nyingine Za Leo Kabla ya pambano la usiku la Ngorongoro Heroes, mapema leo zitapigwa mechi mbili za kukata na shoka:
-
Uganda vs Djibouti: Saa 8:00 mchana (Kundi B)
-
Sudan Kusini vs Burundi: Saa 11:00 jioni (Kundi C)