Ismail Mgunda Afunguka Baada ya Kupewa Nafasi Simba SC
Kitendo cha Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, kumpa nafasi mshambuliaji Ismail Mgunda kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) dhidi ya Mighty Wanderers, kimepokelewa kwa uzito mkubwa na mchezaji huyo, huku akiamini ni mwanzo mzuri wa kuonyesha makali yake.
Mgunda ameeleza kuwa mechi za kimataifa za CAF zina ushindani wa hali ya juu, hivyo kuaminika na kocha Barker kunamjengea kujiamini zaidi na kumpa morali ya kuzidi kujituma ili kuendelea kuwa muhimili ndani ya kikosi hicho.
“Ilikuwa mechi nzuri kwani tumepata ushindi wa kishindo. Binafsi kupata nafasi ni faraja kubwa na inanipa morali ya kupambana nikiamini mechi zinazokuja nitafanya vizuri zaidi,” alisema Mgunda.
Mchezaji huyo aliongeza kuwa jambo la msingi kwake si idadi ya dakika anazocheza, bali ni kutumia vyema muda wowote anaopewa uwanjani.
“Haijalishi nimecheza dakika ngapi, jambo la msingi ni kupata muda wa kucheza na kuonyesha kiwango ambacho kitaendelea kumshawishi kocha aendelee kunipanga,” aliongeza.
Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1, Mgunda aliingia kuchukua nafasi ya Elie Mpanzu na kufanya athari ya haraka baada ya kutoa pasi ya bao (assist) dakika ya 88 lililofungwa na Keletso Makgalwa.
Takwimu za Ismail Mgunda:
-
Msimu wa 2023/24: Alifunga mabao 6 akiwa na Singida Big Stars.
-
Msimu wa 2024/25: Alicheza Ligi Kuu ya Congo (DRC) katika klabu ya AS Vita.
-
Msimu wa 2025/26: Alimaliza msimu akiwa na mabao 2 kabla ya kujiunga na Simba SC kutokea Mashujaa FC.