Rekodi za CECAFA U-20: Kelvin John na Sydney Lokale Watikisa Historia
Wakati michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U-20) ikiendelea kutimua vumbi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, macho na masikio ya wapenzi wa soka yapo kwa wafungaji mahiri wanaosaka heshima ya ufungaji bora.
Katika historia ya michuano hii tangu mwaka 2010, kuna rekodi mbili kubwa za ufungaji ambazo hadi leo zimebaki kuwa tishio na hazijavunjwa.
1. Rekodi ya Kipekee ya Kelvin John (Hat-Trick Mbili Tofauti)
Mshambuliaji wa Kitanzania, Kelvin John, anashikilia rekodi ya kipekee ya kuwa mchezaji pekee aliyefanikiwa kufunga Hat-trick katika matoleo mawili tofauti ya CECAFA U-20:
-
Mwaka 2019 (Uganda): Kelvin alipachika hat-trick yake ya kwanza dhidi ya Zanzibar wakati Ngorongoro Heroes ikiondoka na ushindi wa mabao 5-0. Alifunga mabao hayo dakika za 51, 87 (penalti), na 90.
-
Mwaka 2020: Alirudia tena maajabu hayo wakati Ngorongoro Heroes ilipoichapa Somalia mabao 8-1, akifunga mabao yake dakika za 29, 34, na 48.
Kiwango hiki bora kilifungua milango ya kimataifa kwa nyota huyu ambaye kwa sasa anakipiga kunako klabu ya Aalborg ya Denmark, baada ya kupita KRC Genk ya Ubelgiji.
2. Sydney Lokale: Mfalme wa Mabao Manne Mechi Moja
Kwa upande wa ufungaji wa mabao mengi zaidi kwenye mechi moja, rekodi hiyo inashikiliwa na Mkenya Sydney Lokale.
-
Mwaka 2019: Lokale aliweka historia baada ya kufunga mabao 4 kwenye mechi moja wakati Kenya ilipoichapa Zanzibar mabao 5-0. Mabao hayo yalipatikana dakika za 33, 38, 71, na 80.
Lokale, ambaye amepitia klabu kama Kariobangi Sharks, KCB, AFC Leopards, HIFK (Finland) na soka la DRC na FC Saint Eloi Lupopo, anaendelea kushikilia rekodi hiyo ngumu kufikiwa.
Je, Msimu Huu Rekodi Hizi Zitavunjwa?
Huku mechi zikiendelea kuchezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, swali kubwa kwa mashabiki ni mshambuliaji gani mpya atakayeibuka na kuvunja au kufikia rekodi hizi za Kelvin John na Sydney Lokale.