Yanga Kumpa Mkataba Cedric Kaze: Kutua Kusaidiana na Mngqithi!
UONGOZI wa klabu ya Yanga SC umeingia kwa kasi kwenye mchakato wa kumrejesha kocha wa zamani wa timu hiyo, Cedric Kaze, katika benchi lao la ufundi, huku mazungumzo kati ya pande zote mbili yakitajwa kufikia hatua nzuri ya makubaliano.
Kaze, ambaye anajulikana vyema na mashabiki wa Wananchi kwa mbinu zake na uzoefu wa soka la Bongo na Afrika, anatarajiwa kurejea klabuni hapo ili kuunda safu mpya ya ufundi na kushirikiana bega kwa bega na Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi.
Taarifa za ndani kutoka mitaa ya Twiga na Jangwani zinaeleza kuwa Kaze tayari yupo nchini Tanzania na amekutana na viongozi wa juu wa Yanga. Mambo machache tu ya kimaslahi ndiyo yamebaki kabla ya mkataba huo kutangazwa rasmi kwa umma.
“Mazungumzo yanaenda vizuri sana. Kaze anaijua vyema DNA ya Yanga na soka la Tanzania, hivyo ujio wake utaongeza nguvu kubwa kwenye benchi letu la ufundi,” kilieleza chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga.
Kocha huyo Mburundi kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na klabu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini, hatua inayompa mwanya mwepesi wa kusaini mkataba na Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya NBC.
Uamuzi huu wa Yanga kumpa Kaze mikoba hiyo unakuja wakati timu hiyo ikikabiliwa na ratiba nzito ya michuano ya ndani na kimataifa, ikijumuisha mechi kubwa ya Kariakoo Derby dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC, inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 10, 2026. Ujio wa Kaze unatajwa kuwa chachu ya kuongeza mbinu na utulivu kwenye kikosi cha Mngqithi.