Yusuf Chippo Stand United
Habari za michezo

Yusuf Chippo Adondoka Stand United, Apewa Mkataba Mpya na Mzito!

Vardo September 21, 2026 9:28 am

SHINYANGA, TANZANIA – Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mkenya Yusuf Chippo, amefikia makubaliano rasmi ya kujiunga na kikosi cha Stand United ‘Chama la Wana’ cha mjini Shinyanga kwa ajili ya kupambania nafasi katika Ligi ya Championship msimu wa 2026/2027.

Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Tanzania—akiwa amezifundisha timu kama Pamba Jiji, Coastal Union, na TRA United (zamani Tabora United)—ametua kikosini hapo akitokea Mtibwa Sugar baada ya kukamilisha msimu wa 2025/2026.

Mkataba wa Mwaka Mmoja na Lengo Kuu

Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo amethibitisha kuwa tayari yupo nchini na taratibu za mwisho za uongozi zinakamilishwa kabla ya kuanza kazi rasmi.

“Ni kweli nipo Tanzania kwa ajili ya kujiunga na Stand United. Makubaliano ya awali ni ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja. Malengo makuu ni kuipambania timu hii ili iweze kupanda daraja kutoka Ligi ya Championship hadi Ligi Kuu Bara,” amesema Chippo.

Rekodi na Lengo la Stand United

Chippo alijiunga na Mtibwa Sugar Novemba 17, 2025, akitokea Murang’a SEAL ya Kenya. Katika msimu wa 2025/2026, Mtibwa Sugar ilimaliza nafasi ya 15 ikiwa na pointi 27 (kushinda mechi 6, sare 9, na kupoteza 15).

Pia, kocha huyo anakumbukwa sana kwa mafanikio yake nchini Kenya ambapo aliiongoza Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kati ya msimu wa 2003 na 2005, pamoja na kuhudumu kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars) kuanzia mwaka 2008 hadi 2011.

Jukumu kubwa linalomkabili Mkenya huyo sasa ni kuirejesha Stand United Ligi Kuu Bara, baada ya timu hiyo kushuka daraja tangu msimu wa 2018/2019 iliposhika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 44.

Pigo Zito Kagera Sugar: Mchezaji Nje Msimu Mzima, Wengine 5 Wajeruhiwa! Ngorongoro Heroes Nusu Fainali CECAFA U-20: Mastaa 5 Hatari Waifukuzisha AFCON!