Tanzania vs Burundi AFCON U-20
Michezo Bongo

Tanzania vs Burundi AFCON U-20: Ngorongoro Heroes Kusaka Tiketi ya Fainali Leo!

Vardo September 22, 2026 9:01 am

Vita ya kuwania nafasi za kufuzu Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (AFCON U-20) mwaka 2027 nchini Ghana inafikia tamati leo katika Hatua ya Nusu Fainali ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Pambano kuu linazikutanisha timu mbili zenye rekodi za kuvutia: Tanzania (Ngorongoro Heroes) itakayowakaribisha Burundi saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mchezo mwingine wa nusu fainali utakuwa kati ya Uganda na Sudan.

Timu mbili zitakazotinga Fainali ndizo zitakazopata tiketi ya moja kwa moja kuiwakilisha CECAFA kwenye AFCON U-20 nchini Ghana.


Rekodi Safi za Pande Zote Mbili

Ngorongoro Heroes ilianza kampeni zake kwa kutoa dozi nzito kwa Rwanda (3-0) na Ethiopia (4-0). Mabao saba bila kuruhusu bao lolote ni dhihirisho kwamba kikosi hiki kina safu kali ya ushambuliaji na ulinzi thabiti.

Kwa upande wa Burundi, nao wameingia nusu fainali wakiwa na rekodi safi baada ya kuifunga Sudan Kusini 4-0 na Kenya 2-0, huku pia wakiwa hawajaruhusu bao lolote kwenye hatua ya makundi.


Mchezo Utakapoamuliwa: Mbinu na Silaha za Timu

Sehemu kubwa ya mchezo huu itategemea uwezo wa Tanzania kuvunja safu ngumu ya ulinzi ya Burundi inayoongozwa na Cadeau Ndayishimiye na Radjabu Nzeyimana.

Ili kupata ushindi, Ngorongoro Heroes itahitaji:

  • Kasi na Ubunifu: Kasi ya Chugaboy na ubunifu wa Casemiro katika kiungo.

  • Nguvu na Umaliziaji: Nguvu ya Kibaila na uwezo wa Sagwe kutumia nafasi eneo la hatari.

Kwa upande wa ulinzi, kina Ninju watakuwa na kazi kubwa ya kumdhibiti nahodha wa Burundi, Amini Nshimirimana, ambaye tayari amefunga mabao 4 katika mechi mbili, pamoja na Sympathique Majidi mwenye mabao mawili.


Nusu Fainali Nyingine: Uganda v Sudan

Nusu fainali ya kwanza itazikutanisha Uganda na Sudan. Timu hizi tayari zilikutana katika Hatua ya Makundi ambapo Uganda, chini ya kocha Laryea Kingston, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuongoza Kundi B. Sudan itakuwa na kibarua cha kurekebisha makosa yake ili kufanya maajabu leo.


Kauli za Wachezaji

Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Arafat Ally, alisisitiza maandalizi yao kuelekea mchezo huo:

“Ni mechi ngumu lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda. Hatujapishana sana na Burundi kwa sababu nao hawajaruhusu bao na wamefunga mengi, kwa hiyo tuna kazi ya ziada kuhakikisha tunapata tiketi ya AFCON.”

Mechi zote mbili kupigwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Nani kuibuka kidedea na kukata tiketi ya Ghana?

De Zerbi Awafungukia Wachezaji Tottenham Baada ya Kipigo cha Aston Villa: “Nimechanganyikiwa!” Kocha Mashujaa FC Anena Mazito Mapumziko ya FIFA | Mipango Upya Ligi Kuu