Hamisi Athuman Azam FC
Michezo Bongo

Hamisi Athuman: Ushindani Azam FC, Manula na Ndoto Zake za Kimataifa

Vardo September 24, 2026 9:08 am

BAADA ya msimu mmoja wa kuitumikia KMC kwa mkopo, mlinda mlango Hamisi Athuman amerejea rasmi kwenye klabu ya Azam FC, akiwa na kiu ya kutumia fursa hiyo kujijenga zaidi na kutimiza ndoto zake za kimataifa. Kipa huyo amefunguka mambo mbalimbali kuhusu kurejea Chamazi, ushindani wa namba na Aishi Manula pamoja na Zuberi Foba, maisha yake ya soka, ugumu wa nafasi ya golikipa na malengo yake makubwa.

MANULA, FOBA NA USHINDANI WA NAMBA

Akizungumzia ushindani wa namba dhidi ya makipa wenzake klabuni hapo kama Aishi Manula na Zuberi Foba, Hamisi amebainisha kuwa wanaishi katika mtindo wa kifamilia wenye upendo na kusaidiana kwa kila namna.

Anaeleza kuwa kocha Florent Ibenge ana mfumo wa mzunguko unaotoa fursa kwa kila golikipa kucheza na kuonyesha uwezo wake.

“Mwalimu wetu anampa kila mtu nafasi kulingana na mchezo husika. Nilicheza mchezo wa kwanza, nikapumzika wa pili, nikacheza wa tatu na wa nne kabla ya Foba kurudi na kuendelea,” alisema Hamisi.

AZAM FC NI CHUO CHA SOKA

Hamisi ameitaja Azam FC kama sehemu sahihi inayojenga misingi bora ya mpira nchini, akibainisha kuwa asilimia kubwa ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu hivi sasa wamepitia kwenye mfumo wa vijana wa klabu hiyo.

“Wewe angalia tu Ligi Kuu utagundua kila timu lazima utakuta wachezaji wawili watatu waliopita Azam. Hapa mchezaji anaandaliwa kwa ajili ya ushindani na anaweza kucheza sehemu yoyote,” aliongeza.

Kuhusu uwepo wa makipa wa kigeni kwenye ligi, alisema iwapo kipa mgeni ana uwezo mkubwa unaowazidi wazawa, inakuwa ni fursa nzuri kwao kujifunza, lakini akiwa amezidiwa uwezo na wazawa inakuwa haina maana kubwa.

KIPA: NAFASI NGUMU ZAIDI KWENYE MPIRA

Katika uchambuzi wake wa kiufundi, Hamisi anasisitiza kuwa nafasi ya golikipa ndiyo ngumu zaidi katika soka kwa sababu kosa dogo linazaa bao, tofauti na nafasi nyingine ambapo wachezaji wanaweza kusaidiana kusahihisha makosa.

“Kwangu nadhani kipa ni nafasi ngumu ndio maana unaona wakati mwingine akili zao haziko sawa kwa sababu ya kazi ngumu iliyopo mbele yao,” alieleza.

Alimalizia kwa kueleza kuwa safari yake ya soka ilianzia kwenye viwanja vya mtaani na kuwatazama makipa wa “Ndondo”, akiamini kuwa juhudi na nidhamu ndizo zitakazomfikisha kwenye malengo yake ya kulinda lango la timu ya taifa siku za mbele.

Fainali CECAFA U-20: Ngorongoro Heroes Yamvaa Sudan Leo, Historia Kuandikwa Uwanja wa Uhuru!