Simba Yatimkia Afrika Kusini: Kambi ya Siku 10, Mechi za Kirafiki na Dabi ya Yanga!
SIMBA SC leo imeondoka nchini kuelekea nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuweka kambi ya siku 10, huku macho na masikio ya mashabiki yakielekezwa kwenye maandalizi makali ya Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga SC inayotarajiwa kupigwa Oktoba 10, mwaka huu.
Wekundu hao wa Msimbazi wameanza safari yao saa 4:45 asubuhi, wakitoka moja kwa moja Dar es Salaam hadi Johannesburg, kabla ya kuunganisha safari kuelekea mji wa Polokwane ambako ndipo watakapoweka kambi yao rasmi.
Akizungumza kuhusu safari hiyo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi kitatumia siku hizo kujenga ushindani na utulivu baada ya mapumziko ya kalenda ya kimataifa.
“Leo tarehe 27, siku ya Alhamisi, tutaondoka saa nne na dakika 45 asubuhi. Safari itakuwa ya moja kwa moja kutoka Tanzania, Dar es Salaam mpaka Johannesburg na kisha kuunganisha Polokwane kambi yetu ya siku 10 ilipo,” amesema Ahmed.
Aliongeza kuwa benchi la ufundi limepanga kucheza angalau mechi mbili za kirafiki zenye ushindani mkali ili kupima uwezo wa kikosi kabla ya kurejea nchini kupambana na Yanga na kufuatia mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya kambi hiyo, Simba itarejea nchini na kuungana na wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Dabi ya Kariakoo ya Oktoba 10.