Mfano wa Messi Kwa Argentina Utoe Fundisho Kwa Samatta na Tanzania
Vaibu lililotawala nchini Argentina wakati wa siku maalum ya kumuaga nahodha wao, Lionel Messi, lilikuwa la kiwango cha juu sana. Matukio hayo hayakubamba nchini mwao pekee, bali yalitawala na kukamata hisia za mashabiki wa soka kote duniani.
Waargentina walilipa jambo lao uzito unaostahili, kiasi cha kuifanya dunia nzima isubiri kwa hamu kushuhudia tukio hilo kupitia runinga. Mashabiki kutoka mataifa mbalimbali walilazimika kukesha hadi alfajiri ili kupata mubashara wa sherehe hizo, huku mataifa mengine yakifuatilia katikati ya shughuli zao za kila siku za utafutaji.
Heshima Inayostahili Kwa Legend
Pasipo kuweka unazi wala ushabiki, Waargentina walikuwa na kila haki ya kumpa Messi heshima hiyo kubwa. Mchango wake ndani ya timu ya taifa na uongozi wake uwanjani umekuwa chachu ya mafanikio makubwa ambayo nchi hiyo imeyapata katika miaka ya hivi karibuni. Ni jambo la busara na heshima kwao kumuaga kwa stahiki zake baada ya kuamua kustaafu soka la kimataifa.
Tukio hili linatakiwa kuwa fundisho kubwa kwa mataifa mengine—ikiwemo Tanzania—juu ya namna ya kuwathamini na kuwaheshimu wanasoka waliotukuka kabla hawajastaafu.
Ndivyo Sivyo Kwa Mbwana Samatta?
Hapa nchini Tanzania, kumekuwa na tabia ya kuwachukulia poa wachezaji nyota waliofanya mambo makubwa. Mfano mzuri ni namna baadhi ya mashabiki na wadau wanavyomfanyia Mbwana Samatta, mchezaji aliyeingia kwenye historia kwa kuiwakilisha nchi kimataifa na kuhamasisha vijana wengi kuamini soka linaweza kubadilisha maisha yao.
Ni muda sasa wa kuachana na ule msemo wa kale unaosema “nabii hakubaliki nyumbani.” Ni lazima tubadilishe mtazamo na kuanza kuwapa heshima na thamani inayostahili wanasoka na wanamichezo wetu wote wanaopambana kuiletea heshima nchi.