Siri ya Mafanikio ya Beyonce na Kelly Rowland Baada ya Destiny’s Child
Ukiwazungumzia Beyonce Knowles na Kelly Rowland, unazungumzia nguzo kuu zilizolibeba kundi la Destiny’s Child—moja ya makundi ya waimbaji wa kike yaliyopata mafanikio makubwa zaidi katika historia ya muziki wa RnB na Pop duniani.
Kundi hilo lililoanzishwa mwaka 1990 huko Texas, Marekani, lilipitia mabadiliko kadhaa ya wanachama. Awali lilijumuisha waimbaji kama LeToya Luckett na LaTavia Roberson ambao walikuja kujitoa. Baadaye Michelle Williams na Farrah Franklin walijiunga, ingawa Farrah naye aliondoka muda mfupi baadaye na kuliacha kundi hilo likiendelea na wanachama watatu: Beyonce, Kelly Rowland, na Michelle Williams.
Mchango wa Wazazi wa Beyonce
Mafanikio ya Destiny’s Child hayakutokea kwa bahati mbaya. Wazazi wa Beyonce walicheza nafasi kubwa:
-
Mathew Knowles (Baba): Alisimama kama meneja wa kundi tangu mwanzo hadi liliposambaratika rasmi mwaka 2006.
-
Tina Knowles (Mama): Alikuwa mbunifu mkuu wa mavazi na mitindo ya nywele. Mpaka leo, Kelly Rowland humwita Tina “mama” kutokana na mchango wake mkubwa kwenye maisha yake.
Wimbo wa ‘Dilemma’ na Mabadiliko ya Ratiba
Mwaka 2002, Kelly Rowland alifanya kolabo ya kihistoria na rap star Nelly kwenye wimbo “Dilemma”. Wimbo huo ulipata mafanikio makubwa na kufikisha tazamio (views) zaidi ya bilioni 1.8 YouTube, ikiwa ni miongoni mwa video chache za Hip Hop kufikia idadi hiyo.
Mafanikio ya “Dilemma” yalibadili mipango yote ya kundi:
-
Uongozi uliharakisha kurekodiwa kwa albamu ya kwanza ya Kelly Rowland, ‘Simply Deep’, iliyokamilika ndani ya wiki tatu tu na kuachiwa Oktoba 2002.
-
Beyonce alilazimika kusogeza mbele albamu yake ya kwanza, ‘Dangerously in Love’, kutoka Oktoba 2002 hadi Juni 2003 ili kumpisha Kelly atumie upepo wa mafanikio ya “Dilemma”.
Solo Career na Mafanikio ya Beyonce
Baada ya kuzindua ‘Dangerously in Love’ mwaka 2003, Beyonce alianza ukurasa mpya wa mafanikio ya kishindo. Hadi sasa, ana albamu nane na ni mshindi wa tuzo 35 za Grammy, akiwa msanii mwenye tuzo nyingi zaidi katika historia. Albamu yake ya Cowboy Carter (2024) ilijipatia tuzo ya Albamu Bora ya Mwaka (Album of the Year).
Urafiki na Marudio ya Jukwaani
Ingawa Destiny’s Child ilivunjika rasmi mwaka 2006 baada ya kuuza zaidi ya rekodi milioni 60 na kushinda tuzo 3 za Grammy, wanachama hao wamebaki kuwa marafiki wa karibu.
Wamewahi kuungana tena na kutumbuiza nyimbo zao maarufu kama Say My Name, Soldier, na Lose My Breath katika matukio makubwa kama:
-
Super Bowl Halftime Show (2013)
-
Tamasha la Coachella (2018)
-
Ziara ya Beyonce ya Cowboy Carter Tour (2025)
Nje ya jukwaa, Beyonce na Kelly Rowland wamebaki kuwa kama ndugu. Kelly alihudhuria harusi ya Beyonce na Jay Z mwaka 2008 nchini New York, huku Beyonce na familia yake wakihudhuria harusi ya Kelly na Tim Weatherspoon mwaka 2014 nchini Costa Rica. Jarida la Billboard liliwataja Destiny’s Child kuwa miongoni mwa makundi matatu bora zaidi ya muziki katika historia ya dunia, huku wakiwa na nyota yao kwenye Hollywood Walk of Fame.