Ali Kamwe Avunja Ukimya Baada ya Kipigo cha Simba kwenye Dabi
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kutokata tamaa kufuatia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo mkali wa Kariakoo Dabi, akisisitiza kuwa matokeo hayo hayafuti ndoto yao ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Yanga ilikubali kichapo hicho katika mchezo wa watani wa jadi uliochezwa Jumamosi iliyopita, matokeo yaliyosababisha wakose pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa. Hata hivyo, Kamwe amewatoa hofu wanachama na kuwahakikishia kuwa bado wana nafasi kubwa ya kurekebisha makosa na kurejea kwenye reli ya ushindi.
Akizungumzia hisia za mashabiki wao, Kamwe alikiri kuwa kufungwa katika dabi kuna maumivu ya kipekee kutokana na ushindani wa kihistoria unaogusa maisha ya kila siku ya mashabiki majumbani, mitaani na hata sehemu za kazi.
“Tusijidanganye kwa kusema kwamba kufungwa dabi ni sawa na kufungwa na timu nyingine yoyote. Hisia zake ni tofauti kwa sababu dabi ni sehemu ya maisha yetu,” alisema Kamwe.
Licha ya maumivu hayo, aliwataka mashabiki kutoruhusu hasira kuwavunja moyo, bali zitumike kama motisha ya kuipa timu nguvu mpya kuelekea michezo ijayo. Amewakumbusha kuwa Yanga bado ina michezo 23 ya ligi iliyosalia, hivyo safari ya ubingwa bado haijaisha.
“Msimu unapoanza, kila taasisi hujiwekea malengo. Lengo la Yanga msimu huu ni kupigania na kutwaa ubingwa wa ligi ya ndani. Hatupaswi kuruhusu matokeo ya mchezo mmoja yatutoe katika mwelekeo wetu,” aliongeza.
Msemaji huyo amevitaka vikosi vya uscbelezaji na benchi la ufundi kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza, haki ya kiushindani ikiwa ni pamoja na kuongeza umakini ili kurejesha furaha kwa wanachama kupitia michezo inayofuata ya ligi na michuano ya kimataifa.