Rushine De Reuck Simba SC
Simba SC

Sababu ya Rushine De Reuck Kuondoka Simba Yatajwa, Ahmed Ally Afunguka

Vardo October 14, 2026 11:30 am

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi sababu za kutokuwapo kwa nahodha wa timu hiyo, Rushine De Reuck, akithibitisha kuwa beki huyo amerejea nchini Afrika Kusini kutokana na changamoto za kifamilia zilizomkabili.

De Reuck alikosekana katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilichoichachafya Mashujaa FC kwa mabao 6-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Licha ya utupu ulioachwa na nahodha huyo, safu ya ulinzi ya Simba haikutikisika huku kiungo Yusuph Kagoma akiziba pengo hilo kwa kiwango cha lami.

Kagoma Awashangaza Wengi Beki ya Kati

Kagoma, ambaye amecheza nafasi ya beki wa kati kwa mara ya kwanza tangu kujiunga na timu hiyo, alionyesha ukomavu mkubwa na utulivu wa hali ya juu kwa dakika zote 90, kitendo kilichomfanya Ahmed Ally amwage sifa tele kwa mchezaji huyo.

“Kwa mchezaji ambaye anacheza namba tano kwa mara ya kwanza, amekuwa na utulivu wa hali ya juu. Hakuna makosa ambayo amefanya kwa dakika zote 90. Maana yake Kagoma ni mchezaji anayeweza kucheza nafasi tofauti,” amesema Ahmed.

Ahmed aliongeza kuwa Kagoma ana uwezo wa kipekee wa kumudu nafasi nyingi uwanjani ikiwemo kiungo mkabaji (namba sita), beki wa kati (namba tano), na kiungo wa kati (namba nane), jambo linalomfanya kuwa silaha muhimu kwa kikosi cha Simba chini ya kocha mkuu Steve Barker.

Sifa kwa Kocha Steve Barker

Aidha, uamuzi wa kocha Steve Barker wa kumwamini Kagoma kwenye eneo hilo nyeti upongezwa kwa kuongeza wigo wa machaguo ya wachezaji (depth squad), huku ikithibitisha kuwa Simba ina wachezaji wenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja pindi dharura zinapotokea.

Msimamo Ligi Kuu: Kocha wa Simba Steve Barker Awasha Moto Mpya