Sakata la Israel Mwenda Yanga Lafika Tamati: Ali Kamwe Afunguka Haya!
Sakata la beki wa pembeni wa klabu ya Yanga, Israel Patrick Mwenda, limefika tamati rasmi baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kupitia mgogoro huo na kutoa uamuzi wa mwisho.
Akizungumzia maamuzi hayo, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kuwa uongozi wa klabu hiyo uliamua kuwasilisha suala hilo kwenye kamati husika ili lachunguzwe na kutolewa maamuzi ya haki kwa mujibu wa taratibu na kanuni za klabu na shirikisho la mpira wa miguu.
Kamwe amefafanua kuwa kamati ilikaa, ikajadili kwa kina na kutoa maelekezo yanayomtaka mchezaji huyo kurejea mara moja katika kituo chake cha kazi huku akitekeleza adhabu na maelekezo yote aliyopewa na uongozi.
“Napenda kuwafahamisha wanachama, mashabiki na wapenzi wote wa Yanga kwamba suala la Israel Mwenda limefikia mwisho kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji,” amesema Ali Kamwe.
Kuanzia sasa, Mwenda anatarajia kurejea rasmi katika majukumu yake ya kuitumikia timu hiyo na kuendelea na mkataba wake. Uongozi wa Yanga unaamini kuwa kurejea kwa mchezaji huyo kutaimiza nguvu ya kikosi na kuendelea kuwapa furaha wanachama na mashabiki wao.
Ufafanuzi huu unakuja kufuatia kusambaa kwa picha na minong’ono ya Israel Mwenda katika mitandao ya kijamii siku za hivi karibuni, jambo lililozua maswali mengi miongoni mwa mashabiki kuhusu hatma yake ndani ya kikosi hicho cha Wananchi.