Haji Manara Aonya Yanga: Wanaume Wamepania, Tusiwe Kama Simba ya Zamani!
Aliyekuwa Msemaji wa Yanga SC, Haji Sunday Manara, amewatolea neno zito Wananchi na kuwataka kuacha kurudia makosa yaliyowagharimu wapinzani wao Simba SC, ambao waliwahi kukaa miaka mitano mfululizo bila kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Manara amewasisitiza kukubali ubora wa watani zao badala ya kutafuta visingizio vya kitoto.
Tahadhari hiyo inajiri kufuatia Yanga kupoteza mchezo mkali wa Kariakoo Derby kwa mabao 2-1 dhidi ya Simba uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Manara amesema kuwa wapinzani wao wamejipanga kwa dhati na wana uwezo mkubwa wa kutawala soka la ndani msimu huu iwapo Yanga haitajitathmini na kujipanga upya.
“Wanaume Wamepania Sana”
Akizungumza kuhusu kiwango cha hivi karibuni cha Simba, Manara amesema baadhi ya mashabiki wa Yanga wanapaswa kuacha tabia ya kudai kuwa mafanikio ya Simba yanatokana na matumizi ya dawa au sindano za kuongeza nguvu. Badala yake, amewataka kutambua kuwa timu hiyo inaonyesha uwezo halisi unaotokana na ari ya wachezaji, maandalizi bora na mbinu za kocha wao, Steve Barker.
“Wanayanga wenzangu, mimi General wa vita, Haji Sunday Manara, narudia tena kuwaambia kuwa hawa Makolo mwaka huu wamepania sana na tusipojipanga watabeba ndoo zote za nchi hii,” alisema Manara.
Ameongeza kuwa kiwango kilichoonyeshwa na Simba katika ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Mashujaa FC ni ishara tosha ya hatari, akivutiwa na kasi, nguvu na jinsi kikosi hicho kinavyocheza kwa kushirikiana dakika zote 90.
Kuhusu Yanga Kuepuka Kipigo KINGINE dhidi ya TRA United
Katika hatua nyingine, Manara alizungumzia uamuzi wa Yanga kusogeza mbele mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya TRA United, akidai kuwa huenda hatua hiyo iliwasaidia kuepuka kipigo kingine kizito, huku akiishukuru bodi kwa kuelewa ombi la klabu hiyo.
Yanga kwa sasa inajipanga kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CFFA ya Madagascar, utakaopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ikiwa na jukumu zito la kurejea kwenye njia ya ushindi.