Siri ya Bao la Ajabu la Bwenzi la Mashujaa Dhidi ya Simba Yafichuka
KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa FC, Selemani Rashid ‘Bwenzi’, amefichua siri ya bao lake la umbali mrefu alilofunga dhidi ya Simba, akisema kuwa uamuzi wake ulitokana na kumwona kipa Mahamadou Kassali akiwa mbali na lango lake.
Bwenzi alifunga bao hilo la kuvutia dakika ya 63, wakati timu yake ya Mashujaa ilipokubali kichapo cha mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Katika mchezo huo, Simba ilipata mabao kupitia kwa Libasse Gueye, Anicet Oura, Morice Abraham, Ismael Toure, na Elie Mpanzu aliyefunga mawili.
Akisimulia tukio hilo, Bwenzi amesema kuwa alipokea pasi akiwa katikati ya uwanja na alipogundua kipa Kassali ametoka eneo lake la hatari, hakusita kupiga shuti kali lililoenda moja kwa moja wavuni.
“Mazoezini huwa najaribu mara kwa mara kupiga mashuti ya mbali. Si kila ninalopiga huwa bao, lakini naona kwa kiwango kikubwa kile ninachokifanya mazoezini kinaanza kunilipa. Ni bahati mbaya tu tumepoteza mechi,” amesema Bwenzi.
Kuvunja Ukame wa Miaka Miwili
Licha ya timu yake kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao, kiungo huyo amesema kufunga bao hilo kumempa morali kubwa ya kuendelea kupambana. Bao hilo limekuwa na kumbukumbu ya kipekee kwani limetosha kuhitimisha ukame wa siku 593 takriban mwaka mmoja, miezi saba na siku 16 bila kufunga bao kwenye Ligi Kuu tangu alipofanya hivyo akiwa na KenGrond FC Februari 2025.
Bwenzi alijiunga na Mashujaa FC mnamo Julai 19, 2025, akitokea KenGold, na sasa anaamini bao hili litakuwa chachu ya kurejesha makali yake kamili uwanjani.