Fountain Gate Babati Polisi Tanzania
Michezo Bongo

Mabadiliko Makubwa Ligi Kuu: Fountain Gate Yarudi Babati, Polisi Tanzania Yatimkia Moshi

Vardo October 16, 2026 7:05 pm

BAADA ya kutumia viwanja vya Black Rhino na Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha kwa miezi minane, timu ya Ligi Kuu ya NBC, Fountain Gate, imetangaza rasmi kurejea mkoani Manyara katika mji wa Babati, huku Polisi Tanzania nayo ikirejea katika uwanja wake wa nyumbani mkoani Kilimanjaro.

Uamuzi huo uliotangazwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) unahusisha mabadiliko ya viwanja vya nyumbani kwa baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026/2027.

Fountain Gate awali ilihamia Arusha mwezi Februari mwaka huu kufuatia ombi maalum la Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla. Hata hivyo, sasa inarejea tena Babati ambapo itatumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.

Polisi Tanzania Yarudi Nyumbani Moshi

Kwa upande wa Polisi Tanzania, imeacha kutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid wa Arusha na sasa inarejea katika uwanja wake wa asili wa Ushirika uliopo Moshi, mkoani Kilimanjaro. Kurudi huku kunafuatia kukamilika kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya uwanja huo, hatua inayowezesha timu hiyo kucheza mechi zake za nyumbani mbele ya mashabiki wake wa asili.

Aidha, TPLB imefafanua kuwa timu za Mbuni FC na IAA SC zinazoshiriki Ligi ya Championship nazo zitacheza michezo yao ya nyumbani katika Uwanja wa Agakhan uliopo Arusha.

Wito wa TPLB kwa Wadau wa Soka

Kupitia taarifa yake, TPLB imewakumbusha wadau, mashabiki na wapenzi wa soka katika mikoa ya Manyara, Arusha, na Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi viwanjani kuipa hamasa timu zao. Bodi imesisitiza kuwa ushiriki mkubwa wa mashabiki unaleta chachu ya ushindani na kuimarisha maendeleo ya soka nchini.

Meridianbet Yaandika Ushindi wa Kijamii Buza kwa Kugusa Familia Zenye Uhitaji Real Madrid na Zanzibar Zasaini Mkataba wa Kihistoria wa Soka