Real Madrid na Zanzibar Zasaini Mkataba wa Kihistoria wa Soka
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anaamini kuwa soka la Zanzibar na Tanzania linapokea mapinduzi makubwa kutokana na ushirikiano mpya baina ya klabu nguli duniani, Real Madrid, na taasisi ya Unicorn Zanzibar Sports Limited.
Akizungumza jana Oktoba 13, 2026, jijini Madrid nchini Hispania wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati ya makubaliano hayo, Dk. Mwinyi alieleza kuwa lengo kuu ni kuanzisha programu maalum za mafunzo ya soka yatakayojikita kwa vijana wa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa kipaji pekee hakitoshi kumfikisha kijana kwenye mafanikio bila uwepo wa mwalimu bora, nidhamu, elimu, miundombinu sahihi, na mfumo unaotambua na kuendeleza uwezo wake.
“Serikali imeendeleza zaidi ya viwanja 30 vya mpira wa miguu katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, na hatua inayofuata ni kuunganisha uwekezaji wa maarifa, mbinu za ufundishaji na uzoefu wa kimataifa ili kuwasaidia vijana kufikia uwezo wao,” alisema Dk. Mwinyi.
Aliongeza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijana wanapata mazingira rafiki ya kukuza vipaji na kutimiza ndoto zao. Hata hivyo, alibainisha kuwa mafanikio ya programu hizi hayatapimwa kwa idadi ya vijana watakaocheza soka la kulipwa pekee, bali kupitia mchango wake katika kujenga nidhamu, kujiamini, na kuheshimu wengine.