Simba SC Yamtangaza Rasmi 15 de Agosto: Mchezo Kuchezwa Bila Mashabiki!
WANASIMBA wamepigwa na butwaa! Klabu ya Simba SC imetangaza rasmi kuwa mchezo wake wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 de Agosto utachezwa bila mashabiki, huku pambano hilo likisogezwa mbele kwa siku moja.
Mchezo huo sasa utapigwa Oktoba 21 mwaka huu, saa 9:00 alasiri kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, badala ya Oktoba 20 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mabadiliko haya yametokana na changamoto za usafiri zilizokikabili kikosi cha 15 de Agosto, ambacho kilishindwa kupata ndege ya kuwafikisha nchini kwa wakati.
Kwa mujibu wa Ahmed, wapinzani hao waliomba ratiba ibadilishwe ili wapate nafasi ya kuwasili, kufanya mazoezi, na kujiandaa vizuri kabla ya kukutana na Wekundu wa Msimbazi.
“Kwa hiyo, Oktoba 21 ndiyo tarehe rasmi ya mchezo huo, ambayo tayari imepitishwa na mamlaka zote husika badala ya tarehe 20 kama ilivyokuwa awali,” amesema Ahmed Ally.
LAKINI KUNA KIPIGO KWA MASHABIKI!
Pamoja na kupata tarehe mpya ya mchezo huo, habari iliyowakuta Wanasimba ni kwamba hawataruhusiwa kuingia uwanjani kuishangilia timu yao.
Ahmed amethibitisha kuwa pambano hilo litachezwa bila watazamaji, maana yake Simba italazimika kupambana na 15 de Agosto kwenye Uwanja wa Uhuru bila sapoti ya mashabiki kutoka jukwaani. Hilo linaweka sura tofauti katika maandalizi ya Wekundu wa Msimbazi kuelekea mchezo huo muhimu wa kimataifa katika harakati zao za kusaka tiketi ya kwenda hatua inayofuata.
Sasa macho na masikio ya Wanasimba yanaelekezwa Oktoba 21, wakisubiri kuona kikosi chao kikifanya nini katika pambano hilo litakalopigwa saa 9:00 alasiri, huku milango ya Uwanja wa Uhuru ikiwa imefungwa kwa mashabiki.