Anathiel Chilambo: Kikosi cha Simba Kipo Tayari Kazi CAF!
Beki mahiri wa kikosi cha Simba SC, Anathiel Chilambo, amewatoa hofu mashabiki na wanachama wa timu hiyo kwa kusisitiza kuwa kikosi kipo katika hali nzuri na kiko tayari kupambana kufa na kupona ili kupata ushindi dhidi ya 15 de Agosto katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani Jumatano hii, Oktoba 21, 2026, kuikabili 15 de Agosto katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo, huku wapinzani wao wakichagua kucheza pambano hilo nchini Tanzania.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Chilambo amewataka wachezaji wenzake kujituma kwa asilimia mia moja na kupambana kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanavuna ushindi wa kishindo nyumbani.
“Kucheza Uwanja wa Uhuru bila mashabiki hakuondoi ukweli kwamba bado tuko nyumbani kwenye nchi yetu. Hii ni fursa kwetu kuzoea mazingira na tunapaswa kuingia uwanjani tukiwa na mtazamo mmoja tu wa kusaka ushindi,” amesema beki huyo.
Aidha, akizungumzia hali yake binafsi, Chilambo amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa afya njema na kuahidi kuongeza juhudi kila anapopewa nafasi ya kuitumikia timu hiyo ili kulipa imani ya benchi la ufundi na mashabiki.
Hata hivyo, ametoa rai kwa mashabiki wa Simba SC kuendelea kuiunga mkono timu yao, akisisitiza kuwa umoja, juhudi na kujituma kwa wachezaji ndiyo ngao kuu ya kufanikisha malengo yao barani Afrika msimu huu.