Yanga Yamtisha CFFA! MVUA YA MBAO Inakuja Jumatano
MSEMAJI wa Yanga SC, Ali Kamwe, ametamba kuwa kikosi chao kiko tayari kushusha mvua ya mabao dhidi ya CFFA ya Madagascar katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumatano hii, huku wakilenga kihistoria kuteleza hadi hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nne mfululizo.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Kamwe amewatoa hofu mashabiki na kueleza kuwa mazoezi yanaendelea kwa kasi kubwa katika Viwanja vya Gymkhana. Amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri ya kujiamini tayari kwa pambano hilo litakalopigwa saa 1:00 usiku katika uwanja wa nyumbani wa Azam Complex.
“Tunataka kuendeleza rekodi yetu nzuri. Maandalizi yanaendelea vizuri na wachezaji wanapambana kuelekea mchezo huo. Tunaenda kukamilisha kazi kwa kupambana ili kupata matokeo mazuri ya jumla na kufuzu hatua ya makundi,” amesema Kamwe kwa kujiamini.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yatakuwa hatua kubwa katika historia ya klabu hiyo na soka la Tanzania kwa ujumla, kwani yataweka rekodi ya kipekee ya kushiriki hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika mara nne mfululizo.
Benchi la ufundi limewasisitiza wachezaji kutumia vizuri kila nafasi ya kufunga itakayopatikana ili kujihakikishia ushindi mnono na kutuma ujumbe mzito kwa vigogo wengine wa soka la Afrika.
“Tumewaambia wachezaji waende wakapambane, ikiwezekana wafunge mabao mengi ili Afrika yote iseme Yanga imeingia hatua ya makundi kwa kishindo kikubwa,” alisisitiza Kamwe.
Mwisho, ametoa wito kwa maelfu ya wanachama na mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani siku ya Jumatano kuipa sapoti timu yao, akiamini hamasa ya mashabiki itakuwa chachu ya ushindi mnono.
3. Vitengo (Categories) vya Kuchagua
-
Michezo
-
Michezo Soka la Bongo
-
Yanga SC