Rushine De Reuck Afunguka: Nia Yake ya Kurejea Timu ya Taifa ya Afrika Kusini
Beki wa nguvu wa klabu ya Simba SC, Rushine De Reuck, bado anaamini kuwa mlango haujafungwa kwake kurejea katika timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana). Nyota huyo anaamini kuwa kiwango chake cha sasa kinatosha kumrejesha kwenye michuano ya kimataifa.
Licha ya kukabiliwa na changamoto ya majeraha yaliyomweka nje ya uwanja kwa vipindi tofauti tangu ajiunge na wekundu hao wa Msimbazi, De Reuck ameendelea kujitengeneza upya ili kurejesha utimamu na ubora wake kamili ndani ya kikosi cha Simba.
Beki huyo wa kati aliwahi kuvaa uzi wa Bafana Bafana mara ya mwisho mwaka 2022 alipokuwa akiitumikia klabu ya Mamelodi Sundowns. Hadi sasa, ameshacheza mechi 17 akiwa na timu hiyo ya taifa, jambo linalothibitisha kuwa ana uzoefu mkubwa wa kutosha katika soka la ushindani la kimataifa.
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, naye amewahi kulizungumzia hili akisisitiza kuwa uzoefu, ubora na uwezo wa De Reuck wa kuongoza safu ya ulinzi ni silaha tosha inayoweza kumsaidia kufikia ndoto zake.
Akizungumzia hilo, De Reuck alisema:
“Bado naamini nina nafasi ya kurejea katika timu ya taifa. Najua uamuzi wa mwisho unategemea benchi la ufundi la Bafana Bafana, lakini bado nina jambo la kukamilisha katika ngazi ya kimataifa.”
Kauli hii inaweka wazi dhamira ya mchezaji huyo kupambana kufa na kupona ili kuimarisha kiwango chake akiwa na Simba SC, huku akiiweka ndoto yake ya kurejea Bafana Bafana hai.